Kiongozi wa Chama cha Maori ameondolewa kutoka kwenye bunge la New Zealand kwa kutovaa tai.
Wabunge wa kiume wanaweza tu kuuliza maswali bungeni humo ikiwa wamevaa tai.
Spika Trevor Mallard alimzuia mara mbili Rawiri Waititi kuuliza maswali. "Sio kuhusu tai, ni kuhusu utambuzi wa kitamaduni," Bwana Waititi alisema wakati anatoka kwenye chumba hicho, vyombo vya habari vya huko viliripoti.
Ametaja tai "kitanzi cha mkoloni" na badala yake amevaa kidani cha jiwe.
Baada ya kuzuiwa kwa mara ya pili, Bw Waititi aliendelea na swali lake hadi Bw Mallard alipomuamuru aondoke kwenye ukumbi huo.
Bw Waititi alisema ametendewa "isivyofaa", na kuongeza kuwa alikuwa amevaa "mavazi biashara ya Maori".
Kiongozi mwenza wa Chama cha Maori, Debbie Ngarewa-Packer, ambaye mwenyewe alikuwa amevaa tai, alimtetea mwenzake lakini hakufaulu.
