Kwa historia haijathibitika kama rekodi za msanii kwenye maisha yake ya nje ya muziki yanaweza kuathiri matokeo ya ushiriki wake kwenye tuzo hizo.
Lakini mfumo wa upigaji kura wa tuzo hizo unahusisha wapiga kura maalumu wanaopatikana kwa kujibu maswali maalum kwenye mtandao wa tuzo hizo kupima uelewa wao kuhuzu muziki na saaa, na wanaofanikiwa kujibu vyema wanakuwa sehemu ya kundi la kupiga kura 500 kupitia BET Academy.
BET Academy inaundwa na wadau kutoka tasnia ya muziki, vyombo vya habari na waandishi wa mitandaoni.
Lakini wenye mawazo mbadala wanaamini kwamba, kwa sasa kwa kuonesha maisha ya nje na rekodi mbalimbali za wasanii inawezekana kuwashawishi wapiga kura hao kufikiria upya kuorodheshwa kwa msanii katika tuzo hizo.
Chris Brown
Msanii wa muziki wa R&B kutoka Marekani ambaye mwaka 2009 alishika vichwa vya habari akishutumiwa kumpiga mpenzi wake za zamani, Rihanna. Alilaumiwa sana kwa kitendo hicho lakini miaka miwili baadae, mwaka 2011 alishinda tuzo nne za BET kati ya sita alizoorodheshwa, ikiwemo ya viwers' choice award.
Hata hivyo, Brown aliomba radhi kwa tukio hilo na akahukumiwa na mahakama kuhudhuria huduma ya ushauri nasaha kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake na akahukumiwa miezi sita kufanya kazi za kijamii.
Alitumia muda mwingi wa Mwaka 2010 kwa makosa ya kumiliki silaha isivyo halali na mwaka 2017 kwa kumtishia mwanamke silaha.
Will Smith
Muigizaji huyu maarufu wa Marekani, alishinda tuzo za BET zaidi ya mara moja na akipewa pia nafasi ya kusherehesha shughuli za utoaji tuzo licha ya kutiwa ndani mwaka 1989 kwa makosa ya kumshambulia mtu ambaye kwa kipigo alichopata karibu awe kipofu. Alishtakiwa kwa makosa ya kushambulia lakini hata hivyo makosa hayo baadae yaliondolewa.
Jay Z
Mmoja wa wasanii maarufu na tajiri duniani, Jay Z, alikutwa na hatia ya kumchoma kisu tumboni mdau mmoja wa muziki kwenye klabu ya usiku wakati huo umaarufu wake ukianza kushika kasi mwaka, mwaka 1999. Alihukumiwa kifungo cha nje cha miaka mitatu. Jay Z pamoja na rekodi hiyo ya jinai , ana karibu tuzo 7 za BET alizoshinda kati ya mwaka 2001 mpaka 2018.
50 Cent
Mwaka 1994 , akiwa na umri wa miaka 19, 50cent alikutwa na hatia ya kuuza dawa za kulevya aina ya heroine na cocaine na kutumikia jela miezi sita.
Mwaka 2002 alihukumiwa kifungo cha nje cha miaka miwili kwa kosa la kushambulia. 50 Cent pamoja na rekodi hizo, ameshashinda karibu tuzo nne za BET zikiwemo mbili alizotwa kwa mpigo mwaka 2003, ya rapa bora wa mwaka na msanii mpya wa mwaka.
Lil Wayne
Ni mmoja kati ya wasanii wengi wa Marekani wanaosifika kwa kujihusisha na makosa ya jinai, amewahi kukamatwa kwa kuvuta bangi hadharani na kukutwa na silaha ya meneja wake kinyume na sheria, ilikuwa mwaka 2007.
Ukiacha makosa ya dawa za kulevya, mara kadhaa alipatikana na hatia ya kukutwa na silaha na kuhukumiwa.
Mara ya mwisho ni mwaka jana, alipokamatwa na silaha lukuki kwenye ndege yake binafsi. Msanii huyu aliachiwa huru kwa msamaha wa rais Donald Trump January 19, 2021, Katika siku yake ya mwisho ya kiongozi huyo madarakani. Hata hivyo Lil Wynne ni miongoni mwa wasanii wachache wa rap waliozoa tuzo zaidi ya 10 za BET.
Michael Vick
Huyu si msanii bali Mchezaji wa zamani wa ligi ya soka la Marekanai (NFL), alishinda tuzo ya BET ya mwanamichezo bora mwaka 2011, baada ya kutumikia miezi 19 gerezaji kwa kosa la kushiriki michezo ya kupigaisha mbwa, ambayo inahusishwa na kamari.
Ukiacha rekodi za jinai wapo wasanii wengi na wanamichezo wengi wenye asili ya Afrika wamewahi kutwaa tuzo hizo za BET na tuzo nyingine licha ya ushiriki wako kwenye makosa hayo na hata kushirikiana au kuwa na ukaribu na watu wenye tuhuma mbalimbali.
Mwaka 2015, wadau wengi wa muziki hasa Afrika, walipaza sauti na hata kuendesha kampeni ya kulalamikia wakitaka wasanii wa Afrika wasibaguliwe kwenye utoaji wa tuzo. Ilionekana wasanii wengi wa Afrika wakikabidhiwa tuzo zao nyuma ya jukwaa badala ya jukwaa kuu, huku wasanii kama Sarkodie, Wizkid, Davido, 2Face na D'Banj wakiwa mstari wa mbele kulalamika.
Baadae Mwakilishi wa BET, Lilian Blankson, alijitokeza na kujibu tuhuma hizo akisema wasanii wa Afrika wanapaswa kuongeza juhudi kwenye sanaa yao na sio kuficha ukweli kuhusu tuzo hizo.




