Bi Coronel Aispuro, alipigwa picha hii mwaka 2019, alipokuwa nje ya mahakama wakati wa kesi ya mumewe alishutumiwa kumsaidia kuongoza genge la Sinaloa
"Ni mwenye hatia," ndivyo alivyojibu Emma Coronel pale jaji wa Marekani alipomuuliza anavyojichukulia katika makosa yanayomkabili ya kumsaidia mume wake, Mmexico JoaquÃn Guzmán maarufu kama "El Chapo", mbabe wa shughuli za ulanguzi wa dawa za kulevya duniani.
Kukiri kwa Colonel kuwa ni mwenye hatia hapo Alhamisi mbele ya mahakama moja nchini Marekani kunatamatisha kungauka kwa mrembo huyo, 31, ambaye amekuwa akiishi na mlanguzi mkubwa wa dawa za kulevya kimataifa.
Hukumu yake imepangiwa kutolewa Septemba 15 na hadi wakati huo ataendelea kuwa korokoroni.
Kosa la kwanza linalo mkabili la kupanga njama ya kugawana dawa za kulevya aina ya kokeini, heroini na dawa zinginezo za kulevya huko Marekani kunaweza kumsababishia kifungo cha maisha gerezani.
Jaji katika kesi hii, Rudolph Contreras, alisema wakati wa kusikillizwa kwa kesi hiyo kwamba hajui ni hukumu gani atakayotoa dhidi ya Coronel ambaye alikanusha kuwa ameahidiwa hukumu ndogo kwa kukubali kukiri makosa yake.
Lakini wataalamu wa sheria wanaamini kuwa Coronel angekabiliwa na wakati mgumu ikiwa angefanyiwa kesi kama mume wake "El Chapo," ambaye sasa hivi anahudumia kifungo cha maisha gerezani nchini Marekani na badala yake alikubali makosa yake kama jaribio la kupunguza kifungo chake gerezani.
"Kukubali mashitaka bila shaka kunatoa matumaini ya kupunguziwa kifungo," Todd Yoder, wakili ambaye ameshughulikia kesi kadhaa za ulanguzi wa dawa za kulevya Marekani, amezungumza na BBC Mundo.
Katika makubaliano ya kukubali kwake kulikotiwa saini na Coronel, waendesha mashitaka walipendekeza kwamba ahukumiwe kifungo cha miezi 108 hadi 135 gerezani.
Dawa za kulevya na pesa
Coronel, ambaye ana uraia mara mbili Mmexico - Mmarekani ni mama wa watoto wawili mapacha watoto aliopata na "El Chapo", na alikamatwa mwezi Februari katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dulles karibu na Washington.
"El Chapo" Guzmán anatumikia kifungo cha maisha gerezani nchini Marekani kwa kuongoza mtandapo wa madawa ya kulevya wa Sinaloa.
Makosa dhidi yake mbali na ulanguzi wa dawa za kulevya ni pamoja na njama ya utakatishaji wa pesa.
Mwendesha mashitaka Anthony Nardozzi alisema Alhamisi wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo kwamba Coronel alisaidia mtandao wa Sinaloa ulioongozwa na mume wake kuingiza nchini Marekani dawa za kulevya zaidi ya kilo 450 aina ya kokaine, kilo 90 za heroini, tani 90 za marijuana na kilo 45 za methamphetamine kati yam waka 2011 na 2017.
Aliongeza kuwa baada ya Guzmán kukamatwa huko Mexico mnamo mwezi Februari 2014, Coronel alihudumu "kama ajenti wa kuwasilisha ujumbe" kwa wanachama wa genge hilo kuhusu ulanguzi wa dawa za kulevya na shughuli za utakatishaji wa pesa.
Nardozzi pia alisema kwamba Coronel alipanga njama pamoja na watoto wa Guzmán na wengineo ya kumtorosha mumewe gerezani kulikofanyika Julai 2015 kupitia njia ya handaki ya umbali wa maili moja kutoka gereza laMexico huko El Altiplano.
Alisema kwamba Coronel alipokea pesa kutokana na kuwasilishwa kwa dawa za kulevya pesa taslim kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha sura yake.
"Mwaka 2007 mshitakiwa aliolewa na Guzmán na kuanzia wakati huo hadi kukamatwa kwake Februari 2021 alikuwa akipokea usaidizi wa kifedha kutoka kwa mume wake" kutokana na mauzo ya dawa za kulevya, Nardozzi alisema.
Aliongeza kuwa Coronel alidhibiti nyumba za makazi na biashara ya nyumba zilizolipiwa na Guzmán na kuzipangisha kwa ajili ya kupata pesa.
Marekani imekuwa ikimchunguza Coronel kwa takriban miaka miwili kabla ya kukamatwa kwakwe, ambako kulitokea alipokuwa anaendelea kupata umaarufu: alionekana kwenye kipindi cha televisheni kilichoangazia jamaa za walanguzi wa dawa za kulevya na alikuwa na mipango ya kuanzsha kampuni yake ya nguo chini ya jina "El Chapo."
Wakati wa kesi ya Guzmán, ambayo alikuwa anaishuhudia kila siku miongoni mwa umma katika mahakama moja huko New York mwaka 2019, kulitokea ushahidi dhidi yake.
Dámaso "El Licenciado" López, mmoja wa mashahidi katika kesi hiyo ambaye alikuwa akiaminiwa sana na "El Chapo", alielezea vile alivyoshiriki katika njama ya kumtorosha mume wake kwa kufanya naye mikutano mara kadhaa.
Ushahidi pia ulionesha kuwa Coronel alikuwa kama mjumbe kati ya mume wake na baba yake, aliyetambuliwa kama mwanachama mwingine wa genge la dawa za kulevya la Sinaloa wakijadiliana kuhusu usafirishaji wa dawa za kulevya.
"Huenda alikabiliwa na shinikizo kali"
Wataalam wanaamini kuwa ikiwa Coronel angeamua kufanya kesi, angekuwa na uwezekano mkubwa wa kuishi siku zake zilizosalia maishani gerezani.
"JAngalia tu kilichomtokea mume wako, mtu ambaye anataka kuonesha kuwa serikali imekosea," amesema Yoder. "Kifungo cha maisha gerezani mara nyingi hutokea baada ya kuamuliwa kwamba una makosa katika kesi za aina hii."
Bi Coronel Aispuro alikamatwa Februari
Sasa hivi jaji ana uwezo wa kumhukumu Coronel kifungo cha miaka chini ya kumi gerezani, hukumu ya kwanza ikitolewa kwa kosa la kwanza la ulanguzi wa dawa za kulevya linalomkabili.
Colonel pia anaweza kufupisha kifungo chake gerezani kwa programu za kubadilisha tabia kwa kuwa yeye ni raia wa Marekani na kulenga kuwa na tabia njema.
Kufuatia kukamatwa kwake, taarifa za vyombo vya habari ziliibuka kutoka kwa vyanzo ambavyo havikutaka kutambuliwa vikisema kuwa Coronel huenda akashirikiana na mamlaka ya Marekani kwa kutoa taarifa kuhusu genge hilo katika juhudi za kupunguza kifungo chake gerezani.
Katika ushauri wa wakili Yoder, kuna uwezekano kuwa Coronel akatoa ushirikiano kwa mamlaka na ingawa bado haijajulikana kama atakubali hilo, makubaliano yaliyotiwa saini ni pamoja na kurejelewa kwa hoja kuwa serikali hupunguza kifungo kwa kutoa ushirikiano.
"Lazima alikabiliwa na shinikizo kutoka kila pembe kwa uhalifu mbalimbali waliodai kwamba alitekeleza na sasa amekubali kuwajibika," Yoder amesema. "Nafikiri haya ni makubaliano mazuri kwake."


