Chato ndio nyumbani kwa hayati John Pombe Magufuli
Hata kabla mwili wa hayati Rais John Magufuli haujaingia kaburini nyumbani kwao alikozaliwa, wazee wa Chato walimpa mtego Rais Samia Suluhu Hassan - wakijua hasa nini ulikuwa muktadha wake katika mila na desturi za Kiafrika.
Machi 26 mwaka huu -katika siku ya mazishi yake na mbele ya mwili wa Magufuli, mwakilishi wa wazee wa Chato, Samwel Bigambo, alimwomba Rais Samia kukamilisha ndoto ya mtangulizi wake ya kufanya wilaya hiyo iliyo ndani ya Mkoa wa Geita kuwa Mkoa kamili.
Katika siku yenye hisia kali, bila shaka Mzee Bigambo akijua analolifanya, Samia aliweza kukwepa mtego huo wa wazee. Katika hotuba yake, alisema kinachotakiwa kwa wilaya hiyo kuwa mkoa ni kutimiza vigezo vilivyopo na kama vigezo havijatimia, wataelekezwa jinsi ya kuvifikia.
Kwa jibu hilo, Samia hakukubali palepale wala hakukataa palepale. Kama angetoa kauli ya kukubaliana na wazee wale, ni wazi kwamba asingeweza tena kubadili mawazo kwa sababu angelaumiwa kwa kutoa ahadi ya uongo mbele ya marehemu.
Lakini, kwa sababu hakukataa moja kwa moja na kuweka wazi uwezekano wa kutimia kwa ndoto hiyo ya Magufuli, fursa imeibuka sasa ya kujadili hasa ni sababu ipi hasa inaweza kutumika kuifanya wilaya hiyo kuwa Mkoa.
Mjadala umekuwa mashuhuri zaidi kutokana na matukio mawili tofauti yaliyotokea wiki iliyopita. Kwanza, ilikuwa ni taarifa kutoka katika mkutano wa Baraza la Ushauri la Mkoa wa Geita (RCC) lililotoa taarifa ya kukubaliana na pendekezo la kuigeuza Chato kuwa mkoa kamili.
Baraza hilo lilipendekeza Chato iwe mkoa wenye wilaya tano; Chato, Kakonko, Bukombe, Biharamulo na Ngara. Kwa kufanya hivyo, Chato itakuwa imemega wilaya mbili; Chato na Bukombe kutoka Mkoa wa Geita, Biharamulo na Ngara kutoka Kagera - ikiwamo kata tatu kutoka Wilaya ya Muleba.
Ushauri huo wa RCC haukupokewa vema na madiwani wa Geita ambao katika kikao chao cha Baraza la Madiwani, walitoa taarifa ya kutokubaliana na uamuzi huo wa kuigawa Geita na kufanya Chato kuwa mkoa.
Madiwani hao waliungwa mkono na waziri mstaafu na mchumi mashuhuri nchini, Profesa Anna Tibaijuka, aliyeandika waraka hadharani kupinga hatua ya kuigeuza Chato kuwa mkoa kamili.
Katika waraka wake huo uliosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, Tibaijuka aliandika kwamba uamuzi wa kuifanya Chato kuwa mkoa "hauna faida zozote kiuchumi" na kwamba lengo lake kubwa ni kuwafurahisha wachache kwa sababu zisizo na mashiko.
Kauli hiyo ya Tibaijuka ilikuwa ya kwanza kutolewa hadharani na kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupinga suala hilo la Chato - ambayo ilijipatia umaarufu wa kipekee wakati wa utawala wa Rais Magufuli.
Chato na Gbadolite
Makamu Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Chadema na mwanasiasa mashuhuri wa Tanzania, Tundu Lissu, alikuwa akipinga hadharani kilichokuwa kikionekana kama upendeleo wa wazi kwa Chato uliokuwa ukionyeshwa na Magufuli.
Katika muda wa miaka mitano tu ya kwanza ya utawala wa hayati Magufuli, Chato ilionekana kupanda chati ghafla; kukijengwa uwanja wa ndege, mabenki, kufunguliwa kwa hifadhi ya taifa na mipango mbalimbali ya kuifanya iwe mji wa kisasa nchini Tanzania.
Lissu alikuwa akifananisha kinachoendelea Chato na kile kilichokuwa kinafanywa na aliyekuwa Rais wa Zaire ya zamani, hayati Mobutu Sesseseko, aliyeonyesha upendeleo wa wazi kwa kijiji alikozaliwa cha Gbadolite; alikopeleka miradi wakati wa utawala wake lakini ikawa haina maana baada ya kifo chake.
Rais Samia Suluhu Hassan
Hata hivyo, ndani ya CCM na Serikali, ilikuwa kama mwiko kuonyesha hadharani upinzani dhidi ya huo ulioonekana kama upendeleo wa wazi kwa eneo alikozaliwa Rais - hadi Tibaijuka alipoibuka kwa mara ya kwanza wiki iliyopita.
Kuelewa nini kilichotokea Chato wakati wa utawala wa Magufuli - katika historia ya marais waliotangulia wa Tanzania kabla yake, hakuna hata mmoja aliyejenga uwanja wa ndege wa kisasa wilayani kwake; kuanzia Julius Nyerere hadi Jakaya Kikwete aliyemtangulia Magufuli.
Kwa Watanzania wengi, ni jambo la kupiga hatua katika uhuru wa mawazo ya wengi kwamba sasa walau hata kuna mjadala kuhusu endapo Chato inafaa au haifai kuwa mkoa. Miezi sita iliyopita, huu haukuwa mjadala ambao wanachama wa CCM au watumishi wa serikali wangeweza kushiriki.
Chato inafaa au haifai kuwa mkoa?
Kama mapendekezo ya RCC ya Geita yatapitishwa, mkoa huo mpya utakuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 30,216 na idadi ya watu milioni 1.6. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Sinyamule, mkoa mpya utakuwa na Kata 87 na vijiji 360.
Kwa mujibu wa Mwongozo wa Uanzishwaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2014 uliotolewa na Ofisi ya Rais (Tamisemi), ili eneo litangazwe kuwa mkoa, linahitaji kuwa na vigezo kadhaa vya kufanikisha hilo.
Vigezo hivyo ni pamoja na kuwa na eneo lenye ukubwa wa kuzidi kilomita za mraba 20,000, idadi ya watu wasiopungua asilimia tatu ya idadi ya watu wote kwenye nchi (takribani watu milioni 1.7 kwa hesabu za sasa) kuwa na wilaya nne na sababu nyingine za kiuchumi na kijiografia.
Kwa kufuata mwongozo huo, kuna maeneo ambako Chato itakidhi kuwa mkoa na kuna maeneo ambako haikidhi vigezo. Kwa hoja za Tibaijuka, kwa mfano, Chato kama wilaya kwa sasa haina hata uwezo wa kujiendesha yenyewe na hivyo kuifanya mkoa ni kuongeza mzigo.
Kuna pia sababu za kijiografia ambako kwa kufanya wilaya kama Kakonko kuwa sehemu ya Chato, kutakuwa na umbali na usumbufu mkubwa kwenye kupata huduma muhimu kuliko ilivyo sasa ikiwa sehemu ya Kigoma.
Suala kubwa zaidi hapa ni kwamba katika vigezo ambavyo Chato inakidhi; ukubwa wa eneo, idadi ya kata na idadi ya watu, kuna maeneo mengi nchini ambayo yana sifa hizo kuliko huko alikozaliwa Magufuli. Endapo ombi la Chato litakubaliwa, serikali itakuwa imefungua maombi mengi kuliko uwezo wake wa kuyamudu.
Mtihani kwa Samia
Tanzania ina historia yake ya kipekee linapokuja suala la kufanya mikoa au wilaya kupanda hadhi kutokana na msukumo wa kiongozi au viongozi fulani. Kwa mfano, mchakato wa mgawanyo wa mkoa wa Rukwa kuwa mikoa ya Rukwa na Katavi ulitokea wakati Mizengo Pinda akiwa Waziri Mkuu na Tamisemi ikiwa chini yake.
Pia, Katiba inampa Rais mamlaka ya kutangaza eneo kuwa mkoa au wilaya endapo vigezo fulani vimefikiwa. Hii ndiyo kusema kwamba Rais Samia, akitaka, anaweza kutangaza Chato kuwa mkoa mara mchakato utakapokamilika na kufika mezani kwake.
Kisiasa, jambo hili linaweza kuwafurahisha akina Mzee Bigambo na wale wanaoamini kwamba ana wajibu wa kufanikisha mambo yaliyokuwa moyoni mwa mtangulizi wake ili kwamba atakayekuja baada yake, aweze kukamilisha yale ambayo yeye (Samia) hakufanikiwa kuyakamilisha.
Mtihani pekee kwa Samia ni kwamba endapo atasikiliza kundi hili, atakuwa na mambo mawili ya kukabiliana nayo; kwanza upinzani kutoka kwa wale wanaoamini kwamba huo ni upendeleo wa wazi kabisa kwa mtangulizi wake na pili watu wa maeneo mengine watakaoona nao ni wakati wa kudai kuwa mikoa kama Chato imekidhi vigezo.
Rais Samia alikwepa mtego wa Mzee Bigambo kule Chato siku ya mazishi ya Magufuli. Pasi na shaka yoyote, atajua pia namna ya kufaulu mtihani huu.

