Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo anatarajiwa kurejea nchini humu leo kwa mara ya kwanza tangu alipokamatwa na kuwasilishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai, ICC mnamo mwezi Novemba mwaka 2011 kutokana na jukumu lake katika ghasia za baada ya uchaguzi ambazo zilisababisha vifo vya maelfu ya watu. Tovuti ya Koaci imeripoti.
Ndege ya Gbagbo kutoka Brussels inatarajiwa kutua mjini Abidjan saa 1545 gmt.
Mamlaka za Ivory Coast zimeahidi kwamba atapokelewa "kwa heshima zote kutokana na hadhi ya ofisi aliyoshikilia nchini".
Kurejea kwa Gbagbo kunatarajiwa kupiga jeki chama chake cha Ivorian Popular Front ambacho kinakabiliwa na mgawanyiko kwa miaka kadhaa sasa.
