Mpango mpya wa kuwarejesha masomoni wanafunzi waliopata mimba Tanzania utafanikiwa?

0

 

Elimu

CHANZO CHA PICHA,RADIO JAMBO

Maelezo ya picha,

Karibu watoto 5,000 nchini Tanzania wanatarajiwa kunufaika na mpango wa elimu kwa mfumo usio rasmi katika awamu za mwanzo

Serikali ya Tanzania imetangaza mpango mpya wa kuwarejesha masomoni mabinti waliopata ama wanaopata ujauzito wakiwa mashuleni, mpango ambao utaanza ramsi kuanzia mwaka 2022.

Chini ya utaratibu wa kuboresha elimu ya sekondari Tanzania (SEQUIP), mabinti hao sasa watapata nafasi ya kuendelea na masomo yao waliyokatisha katika mifumo wa elimu wa kawaida.

April mwaka jana, Wizara ya elimu sayansi na teknolojia ilisema tu wanafunzi watanufaika na utaratibu wa SEQUIP, licha ya kugusia lakini haikuwa bayana kwamba wanaopata ujauzito watakuwa sehemu ya wanafukaika hao.

Lakini kupitia kikao rasmi kati ya Katibu mkuu wa wizara hiyo, Leonard Akwilapo na Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya wananchi (FDCs), serikali sasa imetangaza rasmi kwamba wanafunzi wote wa kike waliokatisha masomo yao kwa sababu ya ujauzito watarejea kuendelea na masomo yao kupitia utaratibu huu chini ya mpango wa 'Elimu haina Mwisho'.

FDC

CHANZO CHA PICHA,GOOGLE

Maelezo ya picha,

Moja ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Nandembo FDC, Tunduru, Mbeya

Mpango huu uko chini ya mfumo usio ramsi wa elimu ulioanzishwa tangu mwaka 2008 na Shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania (KTO) ukianza kwa kuwapa elimu mbadala wanafunzi waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali. Mwaka 2017 baada ya Serikali kutangaza marufuku ya wanafunzi wanaopata ujauzito kurejea masomoni mpango huu ukaanza kuwa kama kimbilio kubwa zaidi kunusuru kundi hili la mabinti wanaokatisha masomo yao kwa sababu ya ujauzito.

Kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, mpango huu sasa utatumika rasmi kusaidia mabinti hawa kurejea masomoni. Mkurugenzi wa KTO, Majid Mjengwa amemwambia mwandishi wa Makala haya kwamba mpaka sasa kuna wanufaika 1,185 wa mpango huo ambao wamepata elimu ya sekondari na ujuzi mwingine katika kusaidia maisha yao.

Kwanini Serikali imeamua kupitia Mpango huu usio rasmi?

Baada ya kutangaza kupiga marufuku wanafunzi wanaopata ujauzito kurejea masomoni, kuliibuka mjadala mkubwa nchini Tanzania, wanaopinga hilo wakisema ni kwenda kinyume na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu lakini ni kumnyima moja kwa moja fursa na haki ya elimu binti.

Mjadala huu ulipelekea mpaka Benki ya dunia kusitisha mkopo wake wa dola bilioni 500 kwa Tanzania mpaka itakapopabilisha msimamo wake huo. Lakini baada ya mjadiliano ya muda mrefu sasa kati ya serikali ya Tanzania na Benki ya dunia, wamekubadiliana wanafunzi hao kurejea masomoni na sasa watarejea kupitia mfumo huo usio rasmi chini ya mpango wa elimu haina mwisho.

Elimu

CHANZO CHA PICHA,MICHUZI BLOG

Maelezo ya picha,

Waziri wa elimu, Tanzania, Joyce Ndalichako

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, ni kwamba mpango huu tayari unafanya kazi kwa karibu miaka 14 sasa, hivyo hauitaji kuandikia andiko upya wala kutafuta namna ya kuusimamia na kuutekeleza, kinachofanyika ni kuuboresha ili kukidhi matakwa ya kupokea wanafunzi wengi zaidi kuliko awali.

Mara kadhaa wizara ya elimu nchini humo, kupitia waziri wake, Joyce Ndalichako, imesisitiza umuhimu wa watoto wa kitanzania kupata elimu, na kama serikali itafanya inavyoweza kuhakikisha watoto wengi zaidi hasa wa kike wanapata haki yao ya elimu.

Unafanyaje kazi?

Mpango huu unatumia vyuo vya Maendeleo ya wananchi (FDCs) kusomesha mabinti waliokatiza masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito. Kwa sasa Mpango huo unatekelezwa kwenye vyuo 41 kati ya 55 vilivyopo nchini nzima. Vyuo 14 haviko kwenye mpango huo kikiwemo chuo cha Maendeleo ya wananchi Kibaha ambacho hakiko chini ya Wizara ya elimu bali kiko chini na Shirika la elimu Kibaha.

Lakini sasa Serikali imeagiza vyuo vyote 54 vya FDCs vilivyoko chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuanza kuwadahili mabinti hao kuanzia mwakani.

Akizungumza na wakuu wa vyuo hivyo 54 Katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo aliwataka wasajili vyuo vyao kuwa vituo vya kufanyia mitihani ya kidato cha nne na kidato cha pili ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wa kike walioshindwa kuendelea na masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba wanarudi na kuendelea na masomo.

Wakiwa hapo wanafunzi wa waliopata ujauzito watasoma masomo yao ya sekodari lakini pia wataweza kusoma hata masomo mengine ya ujuzi, yatakayowasaidia katika kuwalea na kuwakuza watoto wao.

Je Mpango huuu utafanikiwa?

Yapo maoni tofauti kuhusu kufanikiwa ama kutofanikiwa kwa mipango ya aina hii.

Ni mpango mzuri, lakini unapaswa kuwekewa mkazo kama ilivyo kwa mfumo maalumu', anasema, Raphael Kugesha, mtaalama wa maendeleo ya Jamii

Hoja inayotajwa zaidi ni kwamba, mfumo huu ni kama unawatenga mabinti hawa na wanafunzi wengine walio katika mfumo rasmi wa elimu.

Maswali mengi ni kuhusu miundo mbinu ya kufudishia na mazingira ya kusomea kwa ujumla kama hayawezi kuwa rafiki kwa binti mdogo mwenye mtoto ama ujauzito anayetaka kutimiza ndoto zake.

FDC

CHANZO CHA PICHA,GOOGLE

Maelezo ya picha,

Kuna jumla ya vyuo 54 vya FDC Tanzania, kimoja kikiwa chini ya Shirika la Elimu Kibaha

Viko vyuo 54 pekee vya maendeleo ya wanachi vitakavyoanza kudahili wanafunzi hawa wa kike kuanzia mwakani, je vitaweza kudahili wanafunzi wote wanaostahili kujiunga navyo kupitia mfumo huu wa elimu usio ramsi kwa wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu ya mimba?

Ingawa serikali inasema, ina uhakika kwa idadi iliyokadiriwa, vyuo hivyo vitaweza kuwapokea wanafunzi hao. Ingawa kwa sasa ziko nafasi 50 zimetengwa kwa kila chuo kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi hao hasa wanatoka mbali, wengi wana wasiwasi na hilo.

Kuhusu walimu, Katibu mkuu wa wizara ya elimu, sayansi na Teknolojia, Akwilapo, alisema' kuhusu walimu tuachieni sisi'.

Wanaoona mpango huo ni muhimu na utafanikiwa wanaonyesha faida yake hasa tofauti na mfumo rasmi.

'Kuna faida kubwa kwenye mfumo huu, kuliko watu wanavyofikiri, mbali na kusoma tu masomo ya sekondari waliyokatisha, watafundishwa pia masuala mengine yatakayowapa ujuzi na kuendesha maisha yao na kulea watoto wao', anasema Mjengwa, Mkurugenzi wa KTO, inayosimamia sasa mpango wa elimu haina mwisho.

KTO

CHANZO CHA PICHA,AFRICA BLOGGING

Maelezo ya picha,

Majid Mjengwa, KTO

Kinachowapa jeuri zaidi wanaouona mpango huu kufanikiwa ni kwamba, wanafunzi hawa watasoma bure lakini pia watapata ujuzi zaidi utakaowasaidia kwenye maisha yao.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya wanafunzi 5,000 wanaweza kudahiliwa mwakani kupitia mpango huu wa kuwarejesha wanafunzi waliokatisha masomo yao kutokana na ujauzito

Kwa utaratibu huu, wanafunzi hawa wakifaulu katika mitihani yao ya kidato cha nne, wataingia kidato cha tano katika mfumo rasmi na kuchanganyika na wanafunzi wengine, Swali linabaki kwa mwanafunzi wa kike wa kidato cha tano akipata ujauzito shuleni, utaratibu wake utakuwaje kuendelea na masomo? Nani atamgharamia? Au ataishia alipoishia na kuendelea na maisha mengine nje ya elimu ya sekondari? Ni maswali yanayohitaji majibu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

About Us

Light Speed Template is Designed Theme for Giving Enhanced look Various Features are available Which is designed in User friendly to handle by Piki Developers. Simple and elegant themes for making it more comfortable