Zaidi ya visa 30,000 vya kuchukuliwa video kisiri vimeripotiwa kwa polisi kati ya mwaka 2013 na 2018
Kyung-mi (ikiwa sio jina lake halisi) alidhalilishwa kwenye mitandao ya kijamii na kudharauliwa na wanaoonea wengine katika mitandao ya kijamii na kuhojiwa na polisi na waendesha mashitaka kwa saa kadhaa baada ya kumshutumu rafiki yake wa kiume ambaye alikuwa maarufu kwa kuchukua video kisiri wakati wanafanya mapenzi.
Alikuwa mwathirika wa uhalifu wa king'ono kwenye mitandao ya kijamii lakini aliambia BBC kwamba "hakuna aliyetaka kumsikiliza".
"Nilikuwa shuleni, nikiwa mdogo na mpweke. Sikuwa na mtu wa kunishika mkono," amesema.
"Nilitamani sana kufariki dunia lakini haikuwezekana," amezungumza na BBC. "Kama ningejitoa uhai hakuna ambaye angejua ukweli kumhusu Jung Joon-young."
Jung Joon-young alianza kuwa maarufu kupitia kipindi cha kwenye televisheni kilichoangazia talanta za watu na alikuwa na wafuasi wengi wa kundi maarufu la muziki la K-pop mashariki mwa Asia.
Kyung-mi anamuelezea mchumba wake kama msikivu na waliopendana - hadi pale alipochukua video kisiri wakati wanafanya mapenzi bila ruhusa yake.
Mara ya kwanza kabisa alipokwenda kituo cha polisi ilikuwa ni Agosti mwaka 2016, lakini anasema maafisa wa polisi walishindwa kupata simu ya aliyeshtakiwa na hatimaye wakaamua kutupilia mbali kesi hiyo.
Alijua kuwa kumshtaki mtu ambaye ni maarufu sio kazi rahisi lakini hakutarajia kwamba angechukuliwa kama mtuhumiwa badala ya mshtaki.
"Maafisa wa polisi waliniambia kwamba nifikirie tena kuhusu taarifa nilizoripoti polisi."
Anasema haikuwa rahisi kumshtaki mtu ambaye ni maarufu dhidi yake.
"Waendesha mashitaka waliniita mimi kuhojiwa, wala sio yeye."
"Nilidhalilishwa, nilitishwa na nikaanza kujiuliza ikiwa mimi ndiye niliyewasilisha kesi."
Jung Joon-young alifungwa jela mwaka 2019
Ilichukua miaka mingine mitatu kabla ya ukweli kubainika kesi kuwasilishwa mahakamani.
Polisi walipata fununu ya video kwenye simu yake mwaka 2019 na hatimaye wakatoa kibali cha kukamatwa kwake.
Walibaini kwamba alikuwa amechukuwa kisiri video za wanawake 12 akiwemo Kyung-mi na kuzishirikisha wengine katika kundi la marafiki zake ambao nao pia ni mashahuri.
Sasa hivi anahudumia kifungo cha miaka mitano jela.
Msemaji wa polisi pia naye aliambia BBC kwamba maafisa waliohusika na kesi ya Kyung-mi pia nao wanachunguzwa.
'Maoni haya ya chuki yanaweza kusababisha mwanamke kujiua'
Tangu Jung alipofungwa jela, Kyung-mi amekuwa akiungwa mkono lakini mwaka 2016 alipowasilisha mashitaka yake kuhusu tabia ya aliyemshtaki, ni wachache sana waliomuamini.
Alidhalilishwa kwenye mitandao ya kijamii na marafiki wakamtoroka.
"Rafiki zangu walisema kwamba ninaharibu maisha ya Jung. Haijalishi niliumia kiasi gani, vyombo vya habari vilikuwa vinanizungumzia mchana kutwa.
"Nchi nzima ilikuwa ina nizungumzia mimi. Hakuna aliyenilinda."
Katika mahojiano yake, Kyung-mi alisema:
"Maneno haya ya chuki yanaweza kufanya mwanamke akajiua," alizungumza na BBC.
Kwa bahati mbaya jaribio lake la kuripoti uhalifu wa kingono kupitia njia wa kidijitali kwa mamlaka Korea Kusini sio jambo geni.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekusanya taarifa ya kina kuhusu waaathirika wa unyama huo nchini humo na kubaini kuwa ni vigumu kwao kupata haki.
Uhalifu wa kingono kwa njia ya mtandao umeendelea kuongezeka kote duniani. Unajumuisha hasa wanaume wanaochukua video kisiri dhidi ya wanawake na wasichana wakati wanafanya nao mapenzi na kushirikisha wengine video hizo.
Kwasababu ya uendelevu wa kiteknolojia, kamera hizo mara nyingi huwa ni ndogo mno - ukubwa wa kifungo cha shati na zinaweza kuwekwa kwenye bafu za umma, vyumba vya mahoteli na hata vyumba vya kubadilisha nguo.
Kiwango cha juu cha intaneti Korea Kusini kinaruhusu picha kupakuliwa kwa haraka sana na kusambazwa kwa wengine na wakati fulani huuzwa kwa wanunuzi wa mitandaoni.
Kamera za siri zilizowekwa kwenye vyoo vya umma Korea Kusini
Zaidi ya visa 30,000 za video zilizochukuliwa kisiri viliripotiwa kwa polisi Korea Kusini kati ya mwaka 2013 na 2018.
"Manusura waliohojiwa na BBC walikuwa wamepitia tajriba za kutisha wakiwa mikononi mwa polisi," kulingana na Heather Barr.
"Mara nyingi tu walikuwa wamefurushwa katika vituo vya polisi.
"Walikuwa wamehojiwa kuhusu masuala nyeti katika maeneo ya umma, wamehojiwa kwa saa kadhaa, wakaarifiwa kwamba ni jukumu lao kukusanya ushahidi, wakazungushwa kutoka ofisi moja hadi nyingine, wakanyanyaswa na kuarifiwa kwamba watupilie mbali kesi walizowasilisha polisi na hata kutishwa kushitakiwa kwa kosa la kiuhalifu la kumharibia mtu jina ikiwa hawatatupilia mbali kesi hizo.
"Pia, tulisikia kuhusu polisi kuchukua video za mapenzi ambazo manusura walikuwa wamezitoa kama ushahidi na kuzisambaza katika kituo chote cha polisi ili tu wapate fursa ya kucheza na wafanyakazi wenzao.
"Fikiria hilo wakati pengine tayari unapitia kipindi kigumu sana cha maisha yako. Wataalamu waliozungumza na BBC wamelielezea hili kama mfadhaiko kwa mara ya pili."
BBC iliwasiliana na polisi huko Korea Kusini kupata jibu juu ya madai haya na msemaji akatoa taarifa kamili kwa maandishi ambayo iliashiria kwamba wamechukua hatua kadhaa kukabiliana na suala hilo.
Ilisema kuwa Timu ya Kuchunguza Uhalifu wa Kingono Mtandaoni imeundwa katika kila mji na eneo nchini humo.
"Tumeanzisha vyanzo kadhaa vya uchunguzi na kanuni pamoja na namna ya kulinda waathirika na kuwaunga mkono," taarifa hiyo imesema.
Pia, polisi imeahidi kuelimisha maafisa wake mara kwa mara na kutoa mchunguzi kwa waathirika wa jinsia sawa naye kusaidia wajihisi huru zaidi huku kituo cha kutoa usaidizi kikianzishwa.
'Unaweza kumuua mtu bila silaha'
Kwa wengine, mfadhaiko huu unakuwa ni jambo wasiloweza kulihimili.
Ripoti ya Shirika la Human Rights Watch ambayo inajumuisha utafiti uliofanywa mtandaoni kwa waathirika zaidi ya 500, ulibaini kuwa mfadhaiko unaosababishwa na uhalifu wa aina hii unaweza kusababisha ugonjwa wa sonona na kuleta fikra za kujiua.
Timu husika pia ilihoji waathiriwa kadhaa waliochukuliwa video kisiri kwa kipindi cha zaidi ya miaka minne ikiwemo wazazi wa mwanamke mmoja kijana ambaye alijiua baada ya kupigwa picha kisiri na wenzake akiwa kwenye chumba cha kubadilisha nguo kazini.
Alihisi kwamba hawezi tena kuondokana na unyanyapaa juu ya unyanyasaji wa aina hiyo.
"Unaweza kumuua mtu bila kutumia sialaha," baba yake alizungumza mwaka 2019.
"Uzito wa uovu huo unaweza kuwa sawa lakini athari zake zinaweza kutofautiana baina ya mtu mmoja hadi mwingine - wengine wanaweza kukabiliana nayo, wengine kama binti yangu wanaweza kushindwa kuhimili."
Kyung-mi anataka jamii ya Korea Kusini kufikiria vile wanavyochukulia waathirika wa uhalifu wa kidijitali.
Kumefanyika maandamano yanayodai hatua kuchukuliwa dhidi ya tatizo hilo la kamera zinazofichwa
Alipata faraja nilipokwenda kijijini
"Niliacha shule wakati naendelea kupata matibabu ya kisaikolojia. Nikaamua kwenda kijijini ambako hakuna aliyejua kisa change na kuanza kusoma maelfu ya vitabu kimya kimya nikifiria kwamba inastahili kubadilika.
Kuzungumza na waathirika wengine wa kingono kulinisaidia kupona majeraha niliokuwa nayo moyoni.
"Nilivumilia machungu niliokuwa nayo ikiamini kwamba siku moja ukweli utadhihirika na uelewa katika jamii utaongezeka."
Na kama jibu kutokana na maandamano hayo, baadhi ya sheria zimebadilishwa lakini adhabu kwa wanaopatikana na hatia bado ni ndogo mno.
"Kila manusura na mtaalamu tuliezungumza naye alikuwa amefadhaishwa na kifungo cha chini kinachotolewa kutokana na uhalifu huu.
"Kuchukua video na picha na kuzishirikisha wengine bila idhini ya mtu ni kosa ambalo adhabu yake ni hadi kifungo cha miaka 7 gerezani chini ya sheria husika, na ni wazi kuwa hukumu hiyo mara nyingi inaonekana kutoendana na athari na machungu wanazopitia waathirika."
Ametoa wito kwa serikali kuanzisha tume kutathmini usawa wa hukumu inayotolewa sasa na namna ya kukabiliana na uhalifu wa kingono mtandaoni kikamilifu.
Hilo linaweza kujumuisha kuruhusu waathirika kulipwa fidia mahakami kitu ambacho kwa sasa hakiwezekani.




