Vladimir Putin amekuwa akiiongoza Urusi tangu 2000. Angela Merkel amekuwa akiiongoza Ujerumani tangu 2005. Uhusiano wa Rais huyo wa Urusi na Kansela wa Ujerumani umepitia misukosuko mingi. Ingawa mwanzo walianza vizuri.
Viongozi wanaoinukia
Mwaka 2002, Merkel alikuwa kiongozi wa kilichokuwa wakati huo chama cha upinzani cha Christian Democratic Union (CDU). Putin alikuwa wakati huo rais mpya wa Urusi. Baada ya kukutana na Putin nchini Urusi, Merkel aliwaambia wasaidizi wake kwa utani kwamba amefaulu "mtihani wa KGB" kwani aliweza kutuliziana macho na Putin.
Merkel kama Kansela mpya mtarajiwa
Putin alikuwa na urafiki na aliemtangulia Merkel, Gerhard Schröder, na viongozi hao wawili wameendeleza urafiki wao hadi hii leo. Mnamo 2005, ilikuwa wazi kwamba Merkel ndiye atakaempokonya kiti cha Ukansela Schröder wa Social Democrat. Hivyo Putin alikutana na Merkel katika ubalozi wa Urusi mjini Berlin.

Mwanamke anayejua kusikiliza kwa umakini
Takriban mwaka mmoja baadaye wakati Merkel ameshakuwa Kansela, Putin alisema: "Hatujuani vizuri sana, lakini nimevutiwa na uwezo wake wa kusikiliza," alimuambia mtangazaji wa kituo cha Ujerumani cha MDR kutoka Dresden, akiongeza kuwa uwezo wa kumsikiliza mwengine kwa umakini ni kitu nadra miongoni mwa wanasiasa wanawake.
Je, Putin alijaribu kumtisha Merkel kwa kutumia mbwa?
Sio siri kuwa Merkel anaogopa mbwa. Hata hivyo, Putin alimruhusu mbwa wake mweusi Konni kuranda kwenye eneo alikomkaribisha Kansela huyo mjini Sochi Januari 2007. Je, lengo lake lilikuwa ni kujaribu kumtisha? Hivyo ndivyo anavyodhani Merkel: "Naamini rais wa Urusi alikuwa anajua fika kuwa sikufurahia kuwa karibu na mbwa wake, lakini bado alimruhusu kuwa karibu nasi."
Merkel amrushia Putin maneno ya kejeli
Kufikia 2012, Vladimir Putin alikuwa ameanza kuwaminya waandishi wa habari na wapinzani wa kisiasa. Alipoulizwa juu ya uhuru wa vyombo vya habari wakati alipokuwa mjini Saint Petersburg, Merkel alijibu kwa nia ya kumkejeli kiongozi mwenzake: "Ikiwa nitakasirika kila wakati ninaposoma gazeti, basi nisingeweza kuwa Kansela hata kwa siku tatu," alisema Merkel.