Poland imesema leo imemuita balozi wa Israel Tal Ben-Ari Yaalon, atoe maelezo baada ya taifa hilo la kiyahudi kuikosoa sheria mpya ya Poland ambayo wataalamu wanasema huenda ikazuia madai ya fidia na malipo kwa maovu yaliyofanywa wakati wa vita vya pili vya dunia.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Poland Pawel Jablonski, amesema serikali ya Poland ingependa kufafanua wazi sheria hiyo iliyopitishwa na bunge Alhamisi iliyopita. Jablonski ameiambia televisheni ya TVP kwamba atakutana na balozi wa Israel siku ya Jumatatu kumuelezea kuhusu sheria hiyo.
Ubalozi wa Israel mjini Warsaw uliandika katika ukurasa wa twitter kuwa sheria hiyo mbaya isiyo na maadili itaharibu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
