Rais wa Msumbiji, Phillipe Nyusi amesema Jumuia ya Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika, SADC itakuwa mdau mkubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi, ambao unashamiri kaskazini mwa nchi hiyo.
Akifungua mkutano wa dharura wa jumuia hiyo ya SADC mjini Maputo, Rais wa Msumbiji ambaye ndiye mwenyekiti wake kwa sasa ameelezea mikakati ya Jumuia hiyo kusaidia kupambana na magaidi ambao kwa sasa wamejikita katika jimbo la Cabo Delgado nchini humo.
Katibu Mtendaji SADC, Stergomena Tax, alisema ingawa kwa sasa juhudi kubwa zimepigwa kuhusu ugaidi kwenye eneo hilo , bado hali ya baadaye ni ya kutilisha wasiwasi.
Mbali na ugaidi mkutano huo wa dharura pia unajadili masuala mbalimbali ikiwemo usalama, migogoro na uchumi wa ukanda huo ambao umeathiriwa kwa kiasi kikubwa vibaya na janga la Corona linalokabili ulimwengu kwa sasa.
Katika Mkutano huo wa dharura, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitambulishwa rasmi na Mwenyekiti wa SADC, ikiwa ni mkutano wake wa kwanza kuhudhuruia kama Rais tangu ashike madaraka mwezi Machi mwaka huu kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli.
SADC ina meno ya kukabiliana na ugaidi?
Bado kuna wasiwasi na uwezo wa SADC katika mapambano ya ugaidi katika eneo Cabo Delgado, Kaskazini mwa Msumbiji. Licha ya dhamira yake na nia, huenda ikakabiliwa na upinzani mkali kutokana na nyenzo, mbinu na rasilimali za Jumuia hiyo.
Wengi wanaitazama kama Jumuia inayoweza kushirikiana zaidi kibiashara na kijamii kuliko kwenye masuala ya usalama hasa ugaidi.
Suala la ugaidi nchini Msumbiji halijaanza leo, limeanza tangu mwaka 2017 baada ya wanamgambo wanaodaiwa kuwa ni wakiislam kushambulia mji huo wenye utajiri wa mafuta na gesi wa Cabo Delgado na kusababisha makumi ya watu kuuawa na maelfu kuukimbia mji huo unaokadiriwa kuwa na wakazi 75,000.
Unaweza kujiuliza kwani SADC ilikuwa wapi tangu wakati huo? Au kwa sababu mwenyekiti wake sasa ni Rais wa Msumbiji, maslahi yanafanya suala hilo lishughulikiwe kwa nguvu inayotajwa?
Kuna wakati Umoja wa Mataifa ulisema ulikuwa umepokea taarifa za kuogofya kwamba Tanzania iliwakatalia watu zaidi ya 1,000 waliokuwa wanakimbia mashambulizi ya wanamgambo kaskazini mwa Msumbiji, lichaya kwamba Tanzania ni jirani na mwanachama wa Msumbiji
Tanzania ilijibu mapigo kupitia kwa Waziri wake wa mambo ya ndani, George Simbachawene kwamba, taarifa ya Umoja wa Mataifa haina uhalisia wowote.
'Hakuna uhalisia wowote wa ripoti hii Je unawezaje kuwajua wanapotaka kuvuka kuja upande wa pili, je unawezaje kuwajua kama humo hakuna magaidi, sisi tunaogopa hawa magaidi, tunalinda mipaka yetu na tunapolinda tusitafsiriwe kama tunawazuia wakimbizi'' anasema Waziri Simbachawene.
Utofauti wa namna hii, unazidi kuleta maswali kwamba SADC iko pamoja kushughulikia usalama katika eneo hilo? Lakini wapo wanaoona kuna matumaini hasa kufuatia kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu, ambaye ujirani na Msumbiji unafanya nafasi yake kuwa muhimu zaidi na leo amehudhuria kikao cha kwanza muhimu cha SADC kuhusu Usalama na masuala ya ugaidi Kaskazini mwa Msumbiji.

