Rais wa Tanzania Bi. Samia Suluhu amezindua leo kiwanda cha kusafisha dhahabu jijini Mwanza kinachoitwa Mwanza Precious Metals Refinery.
Kiwanda hicho chenye thamani ys Bilioni 12.2 za Kitanzania sawa na dola za Kimarekani milioni 5.2 katika uwekezaji wake kitasafisha dhahabu yote ya Tanzania.
Aidha kiwanda hiki kinatajwa kuwa kikubwa zaidi kuliko vyote Afrika Mashariki na kazi yake kubwa itakuwa kusafisha dhahabu za kimataifa.
Kwa siku moja kiwanda kina uwezo wa kusafirisha dhahabu kilo 480 na zinaweza kuongezeka mpaka kufika kilo 960 kwa siku katika kiwango cha juu kabisa cha kimataifa, yaani dhahabu ya Tanzania itasafishwa kwa asilimia 99. 9 ambayo ni karibu 100% .
Katika uzinduzi wa kiwanda hicho, Rais Samia amesema ameona kiwanda hicho kuwa cha miujiza wakati alipoingia ndani kukiona. "Nimeoneshwa vigololi vya dhahabu. Vimeingizwa kwenye mitambo ni dakika 3 kama zilitimia, tayari imeshayeyushwa imetengenezwa bar. Kwahiyo ni mtambo ambao ni wa kisasa wa hali ya juu. Wasiwasi wangu upo kwenye upatikanaji wa malighafi kama kwa siku ni kilo 480 ingawa kuna mashine ndogo ambazo zinasafisha kilo 80 kwa siku nadhani ni kuendana na upatikanaji wa malighafi."
Aidha aliongeza kusema kuwa jukumu la serikali sasa ni kuweka sera, sheria ambazo zitawawezesha wachimbaji wachimbe zaidi malighafi ipatikane kwa wingi zaidi.
Mwanza Precious Metals Refinery ni miongoni mwa viwanda vitatu vipya vilivyoanzishwa nchini Tanzania, na sasa nchi hiyo haitasafirisha tena nje ya nchi dhahabu ghafi.
Ni Ubia kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Madini la Taifa STAMICO yenye asilimia 25 na kampuni za Rozella General Trading LLC ya Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) pamoja na Kampuni ya ACME Consultant Engineers PTE Ltd ya Singapore zina ubia wa asilimia 75.
Hatua hii itaiwezesha Serikali ya Tanzania kupata mapato kupitia tozo na mrabaha, kuongeza teknolojia za kisasa nchini na kutoa ajira rasmi zaidi ya 100 na ajira nyingine zaidi ya 300 zisizo rasmi kwa watanzania.
Kuanza rasmi kwa usafishaji wa Dhahabu katika kiwanda cha Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR) ni matokeo ya Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini kuendelea Kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kusafisha, kuchenjua na kuongeza thamani kufanyika ndani ya nchi hiyo.
Uzalishaji wa mwanzo kabisa katika kiwanda hicho ulianza April 21, 2021.
Akizungumza katika uzinduzi huo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Benki kuu sasa itaweza kununua dhahabu kwa mujibu wa sheria.
"Mtambo huu utawezesha.Benki kuu ya Tanzania BOT yetu kuanza kununua dhahabu kwa mujibu wa sheria na hivyo kuwezesha nchi yetu kuwa na amana ya dhahabu yaani Tanzania sasa tutaanza kuwa na 'gold reserve' kwenye BOT yetu".
Akizungumza katika uzinduzi huo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Benki kuu sasa itaweza kununua dhahabu kwa mujibu wa sheria.
"Mtambo huu utawezesha.Benki kuu ya Tanzania BOT yetu kuanza kununua dhahabu kwa mujibu wa sheria na hivyo kuwezesha nchi yetu kuwa na amana ya dhahabu yaani Tanzania sasa tutaanza kuwa na 'gold reserve' kwenye BOT yetu".
Manufaa ya mtambo huu ni yapi?
- Kuongeza mapato ya serikali ya Tanzania kupitia Mrabaha au tozo za ukaguzi na ushuru wa huduma
- Utoaji wa ajira za moja kwa moja ambazo zinakisiwa kuwa ajira 120 zitakuwa za moja kwa moja na ajira 400 ambazo sio za moja kwa moja
- Mtambo huu utawezesha utunzani wa tofali za dhahabu kwa wazalishaji wa ndani na nje
- Mtambo huu utawezesha madini mengine ambata kwa kuainishwa na kuthaminiwa hapa nchini na nimeliona hilo
- Mtambo huu utaiwezesha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanza kununua dhahabu kwa mujibu wa Sheria na hivyo kuwezesha nchi yetu kuwa na amana ya dhahabu.
- Mradi utasaidia kuchochea shughuli za uchimbaji madini kwenye Ukanda wa Ziwa ambako takribani 90% ya dhahabu inazalishwa kwa sasa lakini kwenye Ukanda huu nimeambiwa kutakuwa kuna viwanda vitatu wasiwasi wangu tu ni kwenye upatianaji wa malighafi. Kwahiyo, tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha malighafi kwenye viwanda hivi zinapatikana.
- Mradi huu utachochea shughuli za kiuchumi kwenye Jiji la Mwanza na kujenga mtambo hii Wawekezaji wametenga mtaji wa takribani dola za Kimarekani Milioni 154 sawa na Tsh. Bilioni 346.5 kwa ajili ya kununua dhahabu yote itakayochimbwa kwahiyo kutakuwa na ushindani mkubwa.
Hata hivyo Rais Samia ametoa wito kwa wachimbaji kutumia fursa hii wakati serikali ikiendelea kuimarisha sekta hii ya madini ikiwemo kudhitibi wizi, utoroshaji na biashara ya magendo ya rasilimali zetu za madini.
Kuhusu suala la madini mengine yanayopatikana Tanzania pekee yaani Tanzanite, Rais Samia amesema serikali yake ipo katika hatua za kufanya baadhi ya marekebisho ili kuipa thamani zaidi.
"Kama tunavyojua Mungu aliipendelea nchi yetu Tanzania peke yake dunia nzima. Ni madini yanayopatikana Tanzania peke yake dunia nzima lakini tunavyokwenda sasa ni kama madini yanayochimbwa dunia nzima. Ukienda kwa majirani zetu kuna Tanzanite nyingi tu.
Kuna haja ya kukaa kuitangaza Tanzanite yetu, kuna haja ya kuipa jina ambayo itaipa umuhimu na upekee Tanzanite yetu, lakini pia kuna haja ya kuwa na mfumo wa kuidhibiti.
Kuwe na mashirika ambayo yataidhibiti Tanzanite yetu ili kuwe na mwamvuli mmoja wa kununua Tanzanite yetu. Kwahiyo, nakuomba Waziri kaa na Wawekezaji mtengeneze mfumo ambao utailinda Tanzanite yetu. Nasemea Tanzanite kwa sababu ndio zao pekee na madini pakee tuliyonayo ambayo tunaweza kuweka jina letu pale".
Pia rais ametaka marekebisho yafanyike katika kutoza kodi , Rais Samia amesema VAT kwa madini yanayoletwa kutoka nje idaiwe baada ya kuchenjua, wanaoleta madini kutoka nchi jirani walete yasafishwe halafu kodi zitapatikana baada ya kusafisha malighafi za madini.
Uzinduzi wa kiwanda hiki ambacho ni miongoni mwa vikubwa zaidi barani Afrika kutaifanya Tanzania kuuza nje madini ambayo yamekwisha chakatwa.
Kwa sasa Tanzania inaungana nan chi nyingine za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda na Rwanda kuwa na viwanda vya kuchakatia dhahabu zake.
Kiwanda kikubwa zaidi Afrika ni Rand Refinery kinachopatikana nchini Afrika Kusini ambacho ni miongoni mwa viwanda vikubwa zaidi duniani kikiwa na uzalishaji wa tani za dhahabu 600 kwa mwaka.

