Katika toleo lililopita tulisimulia jinsi Serikali ya Marekani ilivyopata habari kuwa vita imezuka katika Mashariki ya Kati ikiwahusisha Israel na baadhi ya mataifa ya Kiarabu, ilianza kufuatilia kwa karibu kila habari iliyotoka Mashariki ya Kati.
Waliokutana kujadili kwa kina vita hivyo ni Rais wa Marekani, Lyndon Johnson (1963–1969); mshauri wake wa masuala ya usalama, Walt Rostow (1966–1969); Waziri wa Ulinzi, Robert McNamara (1961–1968); Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Arthur Goldberg (1965 – 1968); Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), Richard Helms (1966–1973) na Mwenyekiti wa Wanadhimu wa Jeshi la Marekani, Earle Wheeler (1964–1970). Mkutano wao ulifanyika katika Ikulu ya Washington.
Hofu ya maofisa wa Marekani ilikuwa ni juu ya Urusi, wakiamini kuwa huenda wangeingilia kati vita hivyo. Saa 1:47 asubuhi jenerali wa zamu kwenye ‘Chumba cha Vita’ katika Makao Makuu ya Jeshi la Marekani (The Pentagon) alimpigia simu McNamara na kumwambia kwamba “Waziri Mkuu Kosygin yuko kwenye ‘laini ya simu’ anataka kuongea na Rais.” Cheo chake kilijulikana kama Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Kisoviet. Alijulikana kama Alexei Kosygin. Simu hiyo iliunganishwa kwenda Ikulu ambako ilipokewa na McNamara.
“Tuseme nini?” McNamara aliuliza.
“Mungu wangu,” lilikuwa jibu la Johnson. “Tuseme nini?”
Kosygin alisubiri kuunganishwa na Rais Johnson, ndipo akasema alichotaka kusema: “Ni jukumu la mamlaka zote kubwa kufanikisha kusitisha mara moja mzozo wa kijeshi (kati ya Israel na nchi za Kiarabu). Serikali ya Soviet imechukua hatua na itachukua zaidi kwa mwelekeo huo. Ni matumaini yetu kuwa Serikali ya Marekani pia itachukua hatua kama hizo na itatoa ushawishi unaofaa kwa Israel.”
Hata hivyo, Kosygin hakujibiwa haraka. Majibu yalikuja nusu saa baadaye wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Dean Rusk (1961 – 1969), alipomweleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Andre Gromyko, jinsi alivyofadhaishwa na habari za mapigano hayo, kisha akamhakikishia kuwa Marekani itafanya kila iwezalo kuhakikisha mapigano hayo yanasitishwa.
“Tunahisi ni muhimu sana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likafanikisha kumalizika kwa mapigano haya haraka iwezekanavyo na tuko tayari kushirikiana na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa,” Gromyko alimwambia Rusk.
Rais Johnson naye akampa Gromyko ahadi yake. Akasema: “Naweza kukuhakikishia kwamba sisi (Marekani) tutatumia ushawishi wetu wote kumaliza uhasama huu.” Pamoja na ahadi hiyo, kulikuwa pia na hali ya kutoaminiana kati ya Urusi na Marekani. Ili kuepuka wasionekane kama wanashirikiana na Israel, Marekani iliamuru meli yake kubwa ya kivita, ikiwa ni pamoja na meli nyingine mbili za jeshi la maji la Marekani zilizokuwa karibu na kisiwa cha Crete, Ugiriki, zisiondoke kama ilivyokuwa imepangwa awali. Pia ilisitisha usafirishaji wa silaha kwenda eneo lolote la Mashariki ya Kati.
Mawasiliano pekee kati ya maofisa wa Marekani na Israel yalipitia kwa Waziri Mkuu wa Israel, Levi Eshkol. Na mawasiliano hayo ni yale tu ambayo hayakuwa ya moja kwa moja na yalifanywa na mtu mmoja tu ambaye ni Harry McPherson. Isitoshe, mawasiliano hayo yalikuwa ni ya mtu na mtu na alisafiri kwenda Israel. Hata hivyo, mazungumzo yao yalikuwa mafupi na kwa ufupi sana.
McPherson aliwahi kuwa mshauri maalumu wa Rais Johnson (1965-1969) na pia alikuwa mwandishi mkuu wa hotuba za Rais (1966-1969). Hata kabla vita haijaanza, mjumbe wa Baraza la Usalama la Marekani, Harold Saunders, Mei 15, 1967 aliishauri Ikulu ya Marekani ifikirie iwapo vita vitaanza kutakuwa na faida yoyote kwa nchi hiyo, hasa kama itachelewa kuingilia kati kwa muda mrefu wa kutosha ili kuruhusu kile walichokiona kuwa ni “ushindi wa dhahiri wa jeshi la Israel”.
Majuma mawili baadaye, Waziri Mdogo wa masuala ya siasa nchini Marekani aliyeshughulikia siasa za Mashariki ya Kati, Eugene Rostow, aliongeza nguvu ya kikosi kazi cha Mashariki ya Kati cha maofisa waandamizi wa kijeshi na wa kiraia na kuwataka waje na “maoni mazuri” juu ya azimio la kumaliza mzozo kati ya Israel na Waarabu.
Rostow aliwaambia maofisa wa jeshi kuwa: “Tusisahau kwamba mgogoro pia ni fursa ... Manufaa mengi hupatikana na milango mingi hufunguliwa. Acheni akili ziende ng’ambo ya upeo wa macho yetu ... Tuangalie fursa zinazoweza kupatikana kutokana na mzozo huu.”
Wakati siku ya kwanza ya vita hivyo ikiwa inaelekea kumalizika, Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani, Walt Rostow, alimwandikia Rais Johnson akipendekeza “Sasa tunapaswa kuanza ... Tunapaswa kuzungumza na Warusi na, ikiwezekana, tuzungumze na wengine kuhusu masharti ya kumaliza mzozo ... Kusitisha mapigano hakutajibu maswali ya msingi yaliyo katika mawazo ya Waisrael hadi pale watakapotwaa sehemu kubwa ya ardhi na kuharibu vifaru na ndege nyingi za Misri. Hapo ndipo tu watakapokuwa na uhakika wa msingi wa majadiliano ya kusitisha mapigano.”
Mabalozi wa nchi za Ulaya waliokuwa Washington waliarifiwa ukweli wa kwamba, “Matukio ya kijeshi ndani ya siku chache zijazo ndiyo yatakayoamua uwezekano wa suluhu ya kidiplomasia juu ya tatizo kubwa la Mashariki ya Kati.” Israel nayo ilitakiwa kutoa maoni yake kuhusu mipango yake baada ya vita.
Mipango ya Rais Johnson ya kuleta amani kati ya Israel na nchi za Kiarabu ambayo ilitoweka mara baada ya kuundwa kwa Taifa la Israel Mei 1948, kisha vita kati ya Israel na baadhi ya majirani zake mwaka 1956 ilielekea kushindwa. Ahadi ya Marekani ya mwaka 1956 ya kuweka jitihada za kuleta amani Mashariki ya Kati haikutekelezwa kwa miaka 11, na kwa hiyo sasa Waarabu hawakuamini ahadi nyingine yoyote kutoka Serikali ya Marekani.
Mabalozi wa nchi za Kiarabu waliokuwa Washington walikataa kuiamini Marekani kwa kauli yake ya kutofungamana na upande wowote katika mzozo huo, wakaishutumu kwamba iliipotosha Misri kwa makusudi ili Israel ipate nafasi ya kushambulia.
Kuanzia Beirut na kwingineko katika nchi za Kiarabu, kulikuwa na maandamano nje ya balozi za Marekani na hata balozi nyingine zilishambuliwa na makundi ya watu wenye hasira.
Hata Marekani kwenyewe hali haikuwa shwari pia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani wa Marekani, Robert McCloskey (1964–1973), alikaririwa akisema: “Msimamo wetu kuhusu vita haufungamani na upande wowote kimawazo, kwa maneno wala kwa vitendo.” Wayahudi wa Marekani walipinga vikali kauli hiyo.
Baada ya hali kuwa tata zaidi, Rusk alilazimika kuingilia kati kufafanua kauli ya McCloskey na kusema “Msimamo wetu wa kutofungamana na upande wowote katika vita hii ni dhana kubwa katika sheria za kimataifa na si usemi unaoashiria kutokujali”.
Baada ya Marekani kubanwa sana, Rusk alilazimika kutoa majibu kupitia jukwaa la Umoja wa Mataifa. Alisema: “Tumesikitishwa na taarifa za mapigano makubwa yaliyotokea Mashariki ya Kati, tukio ambalo tulitaka kulizuia ... Marekani itatumia nguvu zake zote kumaliza mapigano hayo na kuwe na mwanzo mpya wa amani na maendeleo katika eneo hilo. Tunatoa wito kwa pande zote kuliunga mkono Baraza la Usalama kusitisha mapigano haya.”
