Home bongo habari Waliofanyiwa majaribio dawa ya Ukimwi washindwa kesi mahakamani-5
Waliofanyiwa majaribio dawa ya Ukimwi washindwa kesi mahakamani-5
ben
June 18, 2021
Baada ya miaka sita ya mapambano ya kisheria kudai fidia kwa kufanyiwa majaribio ya dawa ya Ukimwi, waathirika saba waliofungua shauri hilo walijikuta wakipoteza kesi yao ya kikatiba.
Mwaka 2014, Watanzania saba waliodai kushawishiwa na kuingizwa katika majaribio ya dawa ya Ukimwi ya Virodene kutoka Afrika Kusini, walifungua kesi ya kikatiba wakiomba Mahakama Kuu itoe matamko kadhaa na amri ya kulipwa fidia ya Sh100,000,000 kila mmoja.
Hawa walikuwa ni Steven William Kimaro, Bahari Sefu, Juto Ramadhani, Ahmed Said Mwiru, Dickson Masena, Octavunus Francis Duya na Mhando Haji Mayuwe
Wajibu maombi katika kesi hiyo namba 32 ya mwaka 2014 walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, makatibu wakuu wa wizara za Afya na Ustawi wa Jamii, Mambo ya Ndani, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na kliniki ya Chadibwa inayomilikiwa na Inspkata Jenerali mstaafu wa Jeshi la Polisi, Omar Mahita.
Waathirika hao waliiomba mahakama itamke kwamba majaribio ya Virodene nchini Tanzania yaliwadhalilisha na kuwavunjia heshima.
Walitaka tamko kuwa matumizi ya miili yao katika majaribio hayo bila kufuata utaratibu unaotakiwa kulikiuka Ibara ya 12 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waathirika hao hao saba kati ya 64 waliofanyiwa utafiti huo, waliiomba mahakama itamke kuwa majaribio hayo yalivunja Ibara ya 13 (6) (e), 14 na ya 29 (2) na kwamba Serikali haikutimiza wajibu wake wa kuheshimu na kulinda haki zao.
Watu hawa ambao tayari walikuwa wakiishi na virusi vya Ukimwi walidai kushawishiwa na madaktari katika hospitali na vituo vya afya visivyo vya kiserikali walikokuwa wakitibiwa na kukubali kufanyiwa majaribio hayo, kwa ahadi kuwa wao na wenza wao watakuwa wa kwanza kupatiwa dawa hiyo bure.
Majaribio hayo ambayo yalikataliwa na Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Binadamu (NIMR) yalidaiwa kufanyika kinyemela katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), Lugalo na zahanati ya Chadibwa iliyoko Ukonga, Dar es Salaam.
Walidai baada ya kupotoshwa na kuamini kuwa utaratibu wote wa kufanyika kwa utafiti huo ulifuatwa na kukubaliwa na Serikali, walikubali kushiriki majaribio hayo kati ya mwaka 2000 na 2001 chini ya usimamizi wa maofisa wa kampuni iliyoitwa Virodene Pharmaceutical Holding (Pty) Ltd.
Waliieleza mahakama kuwa dawa ya Virodene iliyoingizwa katika miili yao iligeuka kuwa sumu na kuwasababishia madhara makubwa kwa afya.
Walisema hapakuwa na hatua stahiki za kuwatibu kufuatia madhara ya dawa hizo, na mbaya zaidi, hawakuwahi kuelezwa kabla ya majaribio kuhusu nini kinaweza kuipata miili yao kufuatia majaribio hayo.
Waliilaumu Serikali pia kuwa licha ya kuwa na taarifa kuhusu upungufu wa majaribio hayo, iliruhusu yaendelee nchini Tanzania kwa kutumia miili yao na ikachelea kuchukua hatua stahiki kuokoa maisha yao.
Wanasema majaribio ya Virodene yalipopigwa marufuku Tanzania na maofisa wa kampuni ya Virodene kufukuzwa nchini mwaka 2001 bila kukamatwa na kushitakiwa, hakukuwa na mpango uliowekwa na Serikali ya kuwafanyia ufuatiliaji wa kitabibu kiasi cha wao kuachwa bila huduma yoyote.
Kesi yao ilijengwa kwenye ushahidi wa nyaraka mbalimbali za mawasiliano zilizoambatanishwa kati kesi hiyo. Mawasiliano hayo yalihusisha wizara ya afya, Virodine Pharmaceutical Ltd, Dr Neema Gideon Simkoko, Hospitali ya JWTZ Lugalo, zahanati ya Chadibwa na Taasisi ya Utafiti wa Dawa (NIMR) na majeshi ya ulinzi na usalama.
Mawasiliano hayo yalihusu maombi ya ruhusa ya kufanya majaribio hayo ya dawa ya Virodene kwa ajili ya matibabu ya Ukimwi. Waliambatanisha pia nakala za magazeti zilizoonesha mjadala wa Bunge kuhusiana na majaribio hayo.
Serikali yajibu
Wajibu maombi katika kesi hiyo hawakupinga kuwa waleta maombi walikuwa ni watu walioishi na virusi vya Ukimwi, lakini walipinga madai mengine yote na kuwataka wathibitishe.
Wajibu maombi pia walida kuwa NIMR chini ya Wizara ya Afya hawakuwahi kutoa kibali kwa majaribio ya dawa ya Virodene kufanyika nchini. Walikana pia kwamba Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na ile ya Mambo ya Ndani zilisaidia kufanyika kwa majaribio hayo.
Mahakama yaachiwa kuamua
Kufuatia hoja za pande zote mbili, mahakama iliachiwa mambo matano ya kuamua; kwanza, kama kweli majaribio ya Virodene yalifanyika kama ilivyodaiwa. Pili, kama Serikali iliruhusu majaribio ya Virodene kufanyika katika hospitali ya Jeshi Lugalo na kliniki ya Chadibwa, na kama waleta maombi walitumika katika majaribio hayo kinyume na utaratibu.
Mahakama pia ilikuwa na kazi ya kuamua kama kuwaweka waleta maombi katika majaribio hayo, kulikiuka ibara za katiba na kama kila mleta maombi alipata madhara kwa kufanyiwa majaribio hayo na alistahili tuzo ya Sh100,000,000 kila mmoja.
Majaji Dk Benhajj Masoud, Elinaza Luvanda na Stephen Magoiga walioamua kesi hiyo, walisema wakati pande zote zikiwasilisha hoja zao kimaandishi mahakamani, hapakuwa na ushahidi wowote, ama wa maneno au kwa kiapo kwenye rekodi.
Suala kubwa lililojitokeza katika hoja za majibu ya wajibu maombi ni kama madai ya waathirika hao yalithibitishwa kwa ushahidi.
Wakaiomba mahakama iamue pia kwenye masuala mengine mawili; kama vidhibiti vinaweza kuambatanishwa na waleta maombi kwenye hoja za kwanza za kimaandishi na kutumiwa na mahakama katika kutoa uamuzi. Pia waliiomba mahakama kuamua kama kesi hiyo ilipaswa kuwa kesi ya kikatiba.
Hii ilikuja baada ya waleta maombi kuwasilisha hati zao za viapo, baada ya kuwa wamewasilisha hoja zao za maandishi baada ya kuomba na kuruhusiwa kufanya hivyo.
Wakati kesi ikiendelea, wakili wao aliomba ruhusa ya kuwasilisha hati za kiapo za ziada kwa ajili ya kurekebisha upungufu wa kukosekana kabisa kwa ushahidi katika hati za kiapo zilizowasilishwa mwanzo.
“Kutoka kwenye mahojiano kwa mashahidi, ilikuwa wazi kuwa kesi ya waleta maombi ilijengwa kwenye madai matupu kuhusu yafuatayo:
Mahakama ilijikita katika kuamua kama uwepo wa majaribio hayo na kama waleta maombi walishiriki kama watu waliokuwa na maambukizi ya Ukimwi; kutafutwa kwao na kuingizwa katika majaribio; kama walifanyiwa majaribio katika Hospitali ya Jeshi Lugalo na kliniki ya Chadibwa.
Pia ilitakiwa kuamua kama waathirika walipata madhara ya dawa; kama kulikuwa na ukiukwaji wa haki kibinadamu.
Mahakama ilisema walalamikaji hao walishindwa kuipa nguvu kesi yao kwa nyaraka yoyote ya kitabibu au nyingine yoyote iliyoainishwa kwenye hati zao za kiapo,” walisema majaji.
Majaji walisema pia hapakuwa na ushahidi wa kuiunganisha Serikali na kliniki ya Chadibwa, na pia madhara ya dawa waliyoyapata wakati wa majaribio hayo.