Katika sehemu ya tatu ya habari ya Watanzania 64 wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ambao miili yao ilitumika kufanyia majaribio ya dawa za kutibu Ukimwi, Virodene, tuliona jinsi Serikali ilivyokana kuwapa kibali watafiti kutoka Afrika Kusini waliofanya utafiti huo.
Tuliona pia jinsi kampuni iliyoendesha utafiti huo, Virodene Pharmaceutical Holdings Ltd ya Afrika Kusini, ilivyotimuliwa nchini baada ya kuwa imefukuzwa pia katika nchi nyingine ilikojaribu kuendesha utafiti kama huo.
Pia tuliona jinsi waathirika walivyohaha bila mafanikio kutafuta kulipwa haki zao baada ya kugundua utafiti ule uliodaiwa kufanyika katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Lugalo na zahanati ya Chadibwa inayomilikiwa na Inspekta Jenerali mstaafu wa Polisi, Omar Mahita kati ya mwaka 2000 na 2001 haukuwa halali.
Juhudi zao za kupata msaada na fidia serikalini ziligonga ukuta na Naibu Waziri wa Afya wakati huo, Dk Aisha Kigoda alilieleza Bunge kuwa njia pekee ya wanaodai kuathirika na utafiti huo ilikuwa ni kwenda mahakamani. Endelea…
Haikuwa rahisi kwa waathirika wa utafiti huo kupata wanasheria na kuandaa kesi ya kikatiba kudai haki yao kwa kuwa suala hili lilihusisha gharama kubwa.
Kwa hali zao, watu hao hawakuwa na uwezo wa kumudu gharama hizo. Hivyo, walibaki gizani wasijue pa kukimbilia licha ya kuamini kuwa utafiti ule uliwadhalilisha na kuwaathiri kisaikolojia
