Afghanistan:Marekani iliondoka kambi ya Bagram usiku bila kuwaarifu wenzao wa Afghanistan

 

taliban

CHANZO CHA PICHA,EPA

Jeshi la Marekani liliondoka Uwanja wa Ndege wa Bagram - kituo chake muhimu nchini Afghanistan - usiku wa manane bila kuwaarifu Waafghani, kamanda mpya wa kituo hicho amesema .

Jenerali Asadullah Kohistani aliambia BBC kwamba Marekani iliondoka Bagram saa 03:00 majira ya eneo hilo Ijumaa, na kwamba jeshi la Afghanistan liligundua masaa kadhaa baadaye.

Bagram pia ina gereza, na inaripotiwa hadi wafungwa 5,000 wa Taliban walibaki katika kituo hicho.

Taliban wamekuwa wakiyachukua maeneo mengi kwa haraka nchini Afghanistan wakati wanajeshi wa Marekani wanapoondoka .

Jenerali Kohistani alisema Jumatatu kwamba vikosi vya Afghanistan vinatarajia Taliban kumshambulia kambi ya Bagram.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kituo hicho cha ndege, alisema tayari alikuwa akipokea ripoti za kikundi hicho kikifanya "harakati katika maeneo ya vijijini" .

Taliban

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

"Unajua, ikiwa tunajilinganisha na Wamarekani, kuna tofauti kubwa," Jenerali Kohistani alisema. "Lakini kulingana na uwezo wetu ... tunajaribu kufanya bora na kadri iwezekanavyo kuleta usalama na kuwahudumia watu wote."

Marekani ilitangaza Ijumaa kuwa imeondoka Bagram, ikimaliza vyema kampeni yake ya kijeshi nchini Afghanistan kabla ya tarehe rasmi ya kumalizika ya Septemba 11, iliyotangazwa na Rais Joe Biden mapema mwaka huu.

Alipoulizwa na AP juu ya kujiondoa kwenye kituo hicho wakati wa usiku msemaji wa jeshi la Marekani Kanali Sonny Leggett alirejelea taarifa iliyotolewa wiki iliyopita kwamba vikosi vya Marekani vilipanga kuondoka kwao kutoka kwa vituo kadhaa kwa kuwasiliana na kuwafahamisha viongozi wa Afghanistan.

Wiki za hivi karibuni zimeshuhudia Taliban ikichukua kwa haraka maeneo mbalimbali wakati wanajeshi wa Marekani wakiondoka, wakiteka wilaya za vijijini na kuzunguka miji mikubwa ya Afghanistan.

Jenerali Kohistani ana askari karibu 3,000 chini ya amri yake - wakilinganishwa na maelfu ya wanajeshi wa Marekani na washirika wake ambao waliwahi kuwa katika kambi hiyo ya kijeshi.

taliban

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Bagram imedhibitiwa na vikosi mbali mbali kwa miaka mingi. Ilijengwa kwanza na Wamarekani, kwa Afghanistan, miaka 1950, kabla ya kujipata chini ya udhibiti wa Soviet wakati la Urusi lilipofanya uvamizi mwaka wa 1979

Baadaye ilichukuliwa na serikali ya Afghanistan iliyoungwa mkono na Moscow na kisha utawala wa mujahideen, kabla ya mwishowe kuchukuliwa na Taliban wakati kikundi hicho kilipoingia madarakani katikati ya miaka ya 1990.

Wakati Marekani ilipovamia Afghanistan mnamo 2001, iliondoa Taliban na kuchukua udhibiti wa uwanja huo wa ndege, na kuubadilisha kuwa kituo kikubwa cha kupambana na Taliban

Wanajeshi wa Afghanistan kutoroka Taliban

Siku ya Jumatatu zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Afghanistan walikimbilia nchi jirani ya Tajikistan baada ya kukabiliana na wanamgambo wa Taliban, maafisa walisema.

Wanajeshi walikimbilia mpaka wa nchi hiyo jirani ili "kuokoa maisha yao wenyewe", kulingana na taarifa ya walinzi wa mpaka wa Tajikistan.

Vurugu zimeongezeka nchini Afghanistan, na Taliban wamekuwa wakifanya mashambulizi na kuchukua maeneo zaidi katika wiki za hivi karibuni.

Kuzidi kwa mashambulizi yao kumejiri wakati huu ambaokipindi cha miaka 20 ya huduma za jeshi la Nato kinafika tamati .

Idadi kubwa ya vikosi vya kigeni vilivyobaki nchini Afghanistan vimeondolewa kabla ya tarehe ya mwisho ya Septemba, na kuna wasiwasi kwamba jeshi la Afghanistan litaporomoka .

Taliban

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Chini ya makubaliano na Taliban, Marekani na washirika wake wa Nato walikubaliana kuondoa wanajeshi wote kwa ahadi ya wanamgambo kutoruhusu al-Qaeda au kikundi kingine chochote chenye msimamo mkali kuhudumu katika maeneo wanayodhibiti.

Kamati ya Usalama ya Kitaifa ya Tajikistan, ambayo inasimamia usalama wa mpaka, ilisema kwamba wanajeshi wa Afghanistan walitafuta hifadhi mapema Jumatatu asubuhi baada ya kupigana na wanamgambo wakati wa usiku, kulingana na shirika la habari la serikali la Tajikstan, Khovar.

"Walinzi wa mpaka wa Tajik kwa sasa wanadhibiti hali katika mpaka wa Tajikistan na Afghanistan," ilisema.

Taliban sasa inadhibiti karibu theluthi moja ya Afghanistan, na inaendelea kukamata maeneo zaidi kila siku.

Mikoa ya Badakhshan na Takhar, ambayo inapakana na Tajikistan, imeshuhudia harakati za hivi karibuni za Taliban kuteka maeneo makubwa

Hii ni mara ya tatu kwa wanajeshi wa Afghanistan kukimbilia Tajikistan katika siku tatu zilizopita na kisa cha tano katika wiki mbili zilizopita. Imefikisha jumla ya wanajeshi waliorejea Tajikistan kufika takriban 1,600.

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani anasisitiza kuwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo vina uwezo kamili kuwazuia waasi, hata hivyo kumekuwa na ripoti za wanajeshi zaidi wanaotafuta hifadhi nchini Pakistan na Uzbekistan kutoroka vita.

Nchi za jirani, pamoja na zile za Asia ya Kati, zinajiandaa kwa wakimbizi ikiwa vita vitaendelea nchini Afghanistan .

Lyse Doucet, mwandishi mkuu wa BBC wa kimataifa, anasema hali ya hofu na kutojua hatima ya maisha yao inatawala watu wengi nchini Afghanistan.

Taliban

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

"Hawana uhakika kuhusu nchi yao inaelekea wapi, hawana uhakika kuhusu kijiji chao au mji au jiji, na hawana uhakika juu ya maisha yao wenyewe na hatima ya familia zao," alisema.

Hata hivyo msemaji wa Taliban Suhail Shaheen aliambia BBC kuwa Taliban hawahusiki na ongezeko la vurugu hivi karibuni.

Alisisitiza kwamba wilaya nyingi zipo chini ya Taliban kupitia upatanishi baada ya wanajeshi wa Afghanistan kukataa kupigana.

Vikosi vinavyoongozwa na Marekani viliondoa Taliban madarakani nchini Afghanistan mnamo Oktoba 2001. Kikundi hicho kilikuwa kikimpa hifadhi Osama Bin Laden na viongozi wengine wa al-Qaeda waliohusishwa na mashambulio ya 9/11 huko Marekani ambayo yalisababisha uvamizi huo.

Rais Biden amesema kujitoa kwa Wamarekani ni haki kwani vikosi vya nchi yake vimehakikisha Afghanistan haiwezi kuwa ngome ya wanajihadi wa kigeni kupanga njama dhidi ya nchi za Magharibi tena.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post