Kauli ya 'Chokochoko' ya Rais Samia yaibua mjadala Tanzania

0

 


Kauli ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya kuwataka wananchi kulinda amani na utulivu wa nchi imezua mjadala mkubwa nchini humo.

Akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Morogoro, Rais Samia alisema kuna chokochoko zimeanza kujitokeza na kuwataka wananchi kuzipuuza na kutozipokea.

“Vijichokochoko vimeanza naomba msivipokee, wanaokuja na vichokochoko walishajua matumbo yao yanajaaje, chakula chao wanatoa wapi, fedha za matibabu wanatoa wapi, nawaomba sana wasiwaingize kwenye huo mkenge kwa sababu pakichafuka ni wewe utakayekaa ndani na watoto, na mama watoto na msijue chakula mtatoa wapi na wala usijue mtoto akiumwa mtakwenda kumtibu na pesa gani,” alisema Samia bila kueleza kwa undani hizo chokochoko ni zipi.

Ingawa hajaeleza bayana kuhusu chokochoko hizo, baadhi ya wanaharakati na wafuasi wa vyama vya upinzani wanahusisha kauli hiyo na vuguvugu la kudai katiba mpya linaloendelea sasa kupitia mitandao na mikutano ya ndani ya kisiasa hasa ya vyama vya upinzani kikiongozwa na CHADEMA.

‘Kama chokochoko ni kudai Katiba mpya, basi tunataka chokochoko’ aliandika Harry Mwala kwenye mtandao wake wa Twitter

Mwanaharakati Maria Sarungi aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter ‘Kila kukicha tunapewa majina mapya, sisi tunachotaka ni katiba mpya itakayotupa haki kwa wote na kuondoa tabaka linalodhani limejimilikisha nchi’.

Kauli iliyoungwa mkono na Aikande C. Kwayu aliyesema amani inatumika kama kisingizio cha kukwepa kusikiliza maoni ya watu.

Lakini kauli hiyo ya Rais Samia, imeungwa mkono pia na baadhi ya watu wakiwemo wafuasi wa Chama chake tawala cha CCM, wakisema amani na utulivu wa nchi ni jambo la msigi zaidi kuliko matakwa mengine kwa sasa ikiwemo katiba. ‘Tunamuunga mkono Rais wetu wananchi tunataka maendeleo hatuna muda wa kupoteza’ aliandika Vuru Jr.

Huku Malewa_Tz akiwakosoa aliowataja wanaoleta chokochoko kwamba hawawezi kujenga hata hoja.

Licha ya Rais Samia kueleza mbele ya wanahabari msimamo wake kuhusu katiba mpya, akitaka kupewa muda wakati huu akiifungua na kujenga uchumi wa nchi hiyo, kwa majuma kadhaa sasa kumekuwa na wito wa kuhuishwa kwa mchakato wa katiba mpya uliosimama tangu mwaka 2014, huku vyama vingine vya siasa vikieleza kutoshiriki katika chaguzi zozote mpaka kupatikane kwa Katiba hiyo. Kwa sasa nchi hiyo inatumia katiba ya mwaka 1977.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

About Us

Light Speed Template is Designed Theme for Giving Enhanced look Various Features are available Which is designed in User friendly to handle by Piki Developers. Simple and elegant themes for making it more comfortable