BUNGE limetaja mbinu zinazotumika kusafirisha dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kubeba mizigo ya kawaida na kuficha ndani ya bidhaa nyingine kama magunia, viroba na maiti na kutaka ushirikiano katika kupambana na suala hilo.
Hayo yamo kwenye taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi ya shughuli zilizotekelezwa kwa kipindi cha Januari, 2021 hadi Januari, 2022.
Katika taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati, Fatma Hassan Toufiq, ikajadiliwa na kisha kupitishwa na wabunge, serikali imeshauriwa kuwekeza katika vitendea kazi vya kisasa vitakavyorahisisha upekuzi na ukamataji wa dawa za kulevya zinazoingizwa nchini kupitia njia mbalimbali lakini pia vitakavyolinda afya za watumishi.
Alitaja njia hizo ni pamoja na kumeza pipi/kete tumboni, kujifunga mwilini, kuweka ndani ya maiti za binadamu, kuficha ndani ya vifaa mbalimbali kama vile mabegi, sabuni, pafyumu, tairi za magari, mipira, soli za viatu, vitabu, vinyago, bidhaa za makopo na kutumia diplomatic bags na njia nyingine nyingi.
Serikali ilishauriwa pia kuweka mikakati maalumu ya kuhakikisha wanaboresha na kusimamia viwango vya usalama kwa kufunga mashine za kisasa zenye uwezo wa kung’amua dawa za kulevya kwenye mizigo ya abiria, vituo vya malori ya mizigo na uwepo wa mbwa maalumu wa kunusa na kubaini dawa za kulevya.