Shirika la Ndege la Precision Air limethibitisha kuwa ndege zake mbili zimeshindwa kufanya safari zake kama kawaida baada ya ndege moja kupata hitilafu na nyingine kulazimika kutua kwa dharura. Precision Air imethibitisha hilo kupitia Taarifa yake leo Februari 03, 2023 ikibainisha kuwa, moja ya ndege zake ilipata hitilafu ya kiufundi hivyo kusababisha kuchelewa na kuahirishwa kwa safari.
Shirika hilo limesema kuwa, ndege nyingine ya Precision Air ililazimika kutua kwa dharura baada ya kugonga kiumbe aina ya ndege kama kunguru au njiwa wakati ikiruka kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma.
“Tunapenda kuwataarifu wateja wetu pamoja na umma kwa jumla kwamba moja ya ndege zetu imepata hitilafu ya kiufundi hivyo kusababisha kuchelewa na kuahirishwa kwa baadhi ya safari zetu.” imesema Taarifa hiyo ya Precision Air
"Katika tukio lingine, ndege yetu yenye usajili namba 5H-PWD ililazimika kutua kwa dharura baada ya kugongana na ndege. (kama njiwa au kunguru) wakati ikiruka kuelekea Dodoma ikitokea Dar es Salaam.
"Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza, tunafanya jitihada za dhati kurejesha safari zetu katika hali ya kawaida." Imeongeza.
Matukio hayo yanajitokeza ikiwa ni miezi kadhaa tangu ilipotokea ajali mbaya ya ndege ya Presicion Air mwezi Novemba mwaka jana ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Bukoba mkoani Kagera na kusababisha vifo vya watu 19.
#KitengeUdates