Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu raia wa Burundi, Abdukarim Ruzociman (25) kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh1 milioni baada ya kukutwa na hatia ya kuingia na kuishi Tanzania bila kibali.
Ruzociman amesomewa hukumu hiyo leo Jumatatu Juni 28, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Evodia Kyaruzi, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
"Mshtakiwa umetiwa hatiani kama ulivyoshtakiwa, hivyo mahakama hii inakuhukumu kulipa faini ya Sh1 milioni na ukishindwa utatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii," amesema hakimu Kyaruzi.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo ameshindwa kulipa fidia hiyo na hivyo kupelekwa gerezani kwa ajili ya kuanza kutumikia kifungo hicho.
Awali, kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mshtakiwa aliiomba mahakama isimpe adhabu kali kwani alikuwa nchini baada ya kudanganywa kwamba Tanzania kuna maisha mazuri.
"Hakimu nilidanganywa na rafiki yangu ambaye ni Mrundi kuwa Tanzania kuna maisha mazuri lakini mpaka nakamatwa sijawahi kupata kazi wala maisha mazuri, hivyo naomba nirudishwe nyumbani Burundi," amejitetea mshtakiwa huyo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Shija Sitta aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mtuhumiwa kwa kuwa hata Watanzania wenyewe wanahitaji kazi na maisha mazuri.
"Naiomba mahakama yako itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaingia nchini bila kufuata taratibu na sheria za nchini zinavyotaka," amedai wakili Sitta.
Akimsomea hoja za awali, wakili Sitta amedai kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo Juni 24, 2021 katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.
Siku hiyo ya tukio, mshtakiwa akiwa eneo hilo alibainika kuingia na kuishi nchini Tanzania bila kuwa na kibali.
