Fahamu kwanini kuna mgogoro kati ya Rais na Idara ya mahakama Kenya


Rais Uhuru kenyatta na jaji mkuu Martha Koome wakipiga picha na majaji wapya aliowateua

CHANZO CHA PICHA,IKULU YA RAIS

Maelezo ya picha,

Rais Uhuru kenyatta na jaji mkuu Martha Koome wakipiga picha na majaji wapya aliowateua

Katika kipindi cha miezi michache iliYopita, katiba ya mwaka 2010 imeshambuliwa kutoka kila upande.

Afisi ya rais imetaka kuwepo kwa uelewa wakati majaji wanapofanya uamuzi wao kwa kutumia vifungu vya sheria huku idara ya mahakama ikiwa na msimamo kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria kama ilivyo.

Katika vita hivi swali ni je , ni nani atakayeibuka mshindi? Katika utata uliopo sasa ,rais Uhuru Kenyatta alidinda kuwateua majaji sita waliofaa kuapishwa baada ya majina ao kupendekezwa na tume ya kuwaajiri majaji JSC.Rais alitoa sababu zake akieleza kwamba uamuzi wake ulitegemea ripoti za vyombo vya usalama kuhusu mienendo ya majaji ambao waliachwa nje.

Rais mwenye mamlaka mengi

Wakenya wameshuhudia rais mwenye mamlaka chungu nzima .

Katiba ya zamani ilikuwa imelimbikiza uwezo mwingi kwa wadhfa na mmiliki wa afisi ya rais zaidi ya vitengo vyote vya serikali.

Rais alikuwa na madaraka na uwezo wa kuteuwa majaji kutoka kiwango cha mahakimu hadi Jaji mkuu, hatua iliowafanya maafisa wa idara ya mahakama kukosa usalama wa kumiliki afisi hizo na hivyobasi kuhudumu chini ya shinikizo ya rais anayewachagua.

Katika ukusanyaji wa maoni kutoka kwa Wakenya , wengi walisema kwamba uwezo huo wa rais ulipaswa kugatuliwa mashinani ili kupunguza uwezo wake katika serikali kuu hadi katika vitengo vingine vya serikali - wakimaanisha bunge na idara ya mahakama.

Wakenya waliamini kwamba Idara ya mahakama iliyo huru itatumika kama ngao kuwalinda.

Mzozo uliopo kati ya rais na Idara ya mahakama

Katika kipindi cha miezi michache iliopita, maamuzi mengi yaliofanywa na afisi ya rais yalipingwa mahakamani na wanaharakati chini ya Masuala yenye Maslahi ya Umma PLI.

Maeneo husika yakiwa kuhusishwa kwa umma katika maamuzi yote yanayofanywa na afisi ya rais.

Baadhi ya maamuzi yaliofanywa na rais ambayo yamepingwa na mahakama kuu yanashirikisha uteuzi wa makatibu tawala , kuendelea kuwateuwa mawaziri bila kufanyiwa ukaguzi baada ya uchaguzi wa mwaka 2017, kufutiliwa mbali kwa uhamisho wa Shirika la nyama KMC kusimamiwa na idara ya ulinzi nchini KDF, kufutiliwa mbali kwa mchakato wa BBI mbali na kufutiliwa mbali kwa agizo nambari moja 2020 la afisi ya rais ambalo lilitaka kuiweka idara ya mahakama chini ya afisi hiyo.

Jaji mkuu mpya Martha Koome

CHANZO CHA PICHA,IKULU YA RAIS

Maelezo ya picha,

Jaji mkuu mpya Martha Koome

Lakini cha kuvutia ni muonekana wa Idara ya mahakama iliojitolea, isioogopa na iliyo tayari kufuata sheria na kuikumbusha afisi ya rais kufuata sheria inapofanya maamuzi yenye maslahi ya umma.

Idara ya mahakama pia imetaka kuonyesha uhuru wake kuhusu suala la jukumu la afisi ya rais katika uteuzi wa majaji wa mahakama kuu na wale wa mahakama ya rufaa.

Itakumbukwa wakati rais alipotoa matamshi ya vitisho ya "we shall revisit" kwamba baada ya uchaguzi wake kufutiliwa mbali na mahakama mwaka 2017, ili kutaka kujua chanzo cha uhasama uliopo kati ya afisi ya rais na ile ya idara ya mahakama.

Uteuzi wa majaji 41 waliopendekezwa ulicheleweshwa kwa takriban miaka miwili huku majaji 34 pekee wakiteuliwa katika orodha hiyo mbali na kutoanzishwa kwa ufadhili wa idara ya mahakama kama ilivyoashiriwa katika kifungu cha 173 cha katiba kama hatua za kutaka kuhujumu huduma na uhuru wa idara ya mahakama.

Afisi ya rais ikielezea sababu za kucheleweshwa kwa uteuzi huo ilisema kwamba baadhi ya watu wenye matatizo ya kimaadili walikuwa wameorodheshwa katika orodha hiyo iliyowasilishwa kwa rais na Tume ya idara ya mahakama JSC, na kwamba rais alikuwa na jukumu la kutowateuwa watu wenye maswali kuhusu uadilifu wao .

Afisi ya rais hivyobasi ilikuwa imependekeza kwa mwenyekiti wa tume ya idara hiyo jaji mkuu aliyeondoka David Maraga kukubali uteuzi wa baadhi yao huku ikiwaacha nje wale wanaotajwa kuwa na matatizo ya kimaadili.

Lakini msimamo wa Maraga kwa afisi ya rais ulikuwa kuamua kusitisha uteuzi huo kabisa iwapo idadi ndogo ingeteuliwa.

Ni wazi kuhusu sheria iliopo katika katiba ya 2010 juu ya uhuru wa huduma ya mahakama kwa kuhakikisha kwamba Tume ya idara ya mahakama JSC ndio yenye uwezo wa kuteua majaji wote 41 huku rais akiwa na mamlaka madogo ya kuwateua na kuwaweka katika gazeti rasmi la serikali.

Kifungu hicho cha 166{1} kinasema na kilitumia neno 'SHALL' kukusudia na 'IN' ikimaanisha kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume ya Idara ya Mahakama JSC , kumzuia rais kuwa na fursa ya kuchagua nani anayeweza kuwa jaji na nani asiyeweza.

Huku kukiwa na makubaliano kuhusu jukumu kubwa la idara ya upelelezi katika kuwakagua wafanyakazi wa umma , na kwamba watu wenye matatizo ya maadili hawafai kuteuliwa , Je rais alikuwa na uwezo gani ?

Ili kuliangazia suala hilo mtu anapaswa kufahamu muundo na uanachama wa tume ya idara ya mahakama kama ilivyo katika kifungu cha 171 cha sheria.

Ambapo rais ana uwezo wa kufanya uteuzi wa moja kwa moja wa maafisa wanne miongoni mwao , Mwanasheria mkuu, wawakilishi wa tume ya wafanyakazi wa umma na maafisa wawili ambao sio mawakili.

Hii ina maana kwamba rais kupitia wawakilishi wake wanaweza kuwafuta kazi kwa maadili hayo hayo kabla ya kuwasilisha majina hayo.

Baada ya majina kuwasilishwa na JSC huku kifungu cha 166 cha sheria kikianza kutumika, mikono ya rais huwa imefungika

Mchakato wa BBI

Wakati wa maadhimisho ya sherehe za 58 za Madaraka Day , rais Uhuru Kenyatta alitoa maoni yake kuhusu umuhimu wa Idara ya mahakama kuelewa kinachoendelea kuhusu BBI na kuendana na matakwa ya raia.

Rais Uhuru Kenyatta alitoa wito kwa Idara ya mahakama kuelewa kuhusu chaguo lililopo na kutilia maanani 'gharama' na 'faida' zitakazopatikana wakati wanapofanya maamuzi ya mahakama.

Rais alikuwa akitoa wito wa kufanyika kwa mjadala wa kitaifa kuhusu faida zilizopo katika BBI na kwamba Idara ya mahakama haifai kuingilia mpango huo .

Jaji mkuu mpya Martha Koome na Rais Uhuru Kenyatta kulia

CHANZO CHA PICHA,IKULU YA RAIS KENYA

Maelezo ya picha,

Jaji mkuu mpya Martha Koome na Rais Uhuru Kenyatta kulia

Hotuba hiyo ya rais ilisababishwa na uamuzi wa mahakama kuu ambao ulifutilia mbali mchakato wa BBI na kusitisha 'reggae' kwa muda.

Ni muhimu kusema kwamba uamuzi huo wa nakala 300 uliotolewa na mahakama kuu ulitokana na mchakato wa BBI ambao haukufuata sheria na wala haukutokana na kilichopo ndani yake.

Majaji hao waliangazia kuhusu jinsi mchakato huo ulivyoanzishwa na waanzilishi wake, huku rais akizungumzia kuhusu kile kilichopo ndani ya mchakato huo.

Majaji hao waliamini kwamba iwapo mchakato huo haukufuata sheria kama inavyohitajika katika katiba basi matokeo yake pia yasingefuata sheria, msimamo ambao mahakama ya juu nchini Kenya ilitumia katika kufuta matokeo ya urais ya mwaka 2017.

Cha kushangaza ni kwamba majaji wawili kati ya wale watano waliotoa uamuzi huo, walikuwa miongoni mwa wale wanne ambao rais aliwachagua kuwa majaji wa mahakama ya rufaa.

Rais wa mahakama ya rufaa jaji Daniel Musinga, wakati wa kikao cha kusikilizwa kwa kesi hiyo , kilichofanyika siku moja tu baada ya sikukuu ya Madaraka Day aliwaonya wanasiasa kutozungumzia kuhusu suala lililopo mbele ya mahakama , ikiwa onyo ya moja kwa moja kwa hotuba ya rais Kenyatta kuhusu BBI wakati wa sikukuu hiyo.

Jinsi rais anavyopima uwezo wake

Kote duniani , afisi ya rais hujaribu kuona mwisho wa uwezo wake , ili kujua ni kwa kiwango gani katiba inaweza kukiukwa kwa maslahi na kuafikia matakwa yake.

Hatahivyo Mahakama lazima isalie kuwa tumaini la mwisho dhidi ya afisi ya rais yenye hujuma ya sheria.

Nchini Kenya kwa mfano baada ya kuidhinishwa kwa katiba mpya rais mstaafu Mwai Kibaki alijaribu kuteua jaji mkuu mpya bila kufuata sheria , hatua ambayo mahakama kuu ilifutilia mbali na mchakato mpya ukaanzishwa ambao ulipelekea kuteuliwa kwa jaji mkuu Willy Mutunga.

Katika kesi hii , afisi ya rais ilijaribu kutumia uwezo wake mkuu lakini mwisho wa siku ni mahakama iliyoibuka kidedea. Kwa ufupi ni kwamba Sheria iliheshimiwa.

Ukiukaji wa maagizo ya mahakama

Rais Uhuru Kenya amekuwa akifanya baadhi ya maamuzi bila kuzingatia maagizo ya mahakama. Na sasa ameonekana kama kutoneshwa kidonda wakati ambapo maamuzi ya mahakama yamekwenda kinyume na matarajio yake.

Kwa mfano suala la kukataa kuwateuwa na kuwachapisha katika gazeti la rsmi la serikali wale ambao anahisi walikwenda kinyume na matakwa yake.

Huku baadhi ya mapendekezo katika BBI yakitarajiwa kuwafaidi pakubwa raia , mapendekezo mengine kama yale ya afisi ya Ombudsman anayeteuliwa na serikali na anayeripoti kwa bunge yanarudisha nyuma hatua za kidemokrasia zilizopigwa.

Aliyekuwa jaji mkuu Maraga alikuwa mwiba kwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta
Maelezo ya picha,

Aliyekuwa jaji mkuu Maraga alikuwa mwiba kwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta

Watengenezaji wa katiba mpya walienda umbali wa kulinda uhuru wa Idara ya mahakama . Kifungu cha 159[1] na kifungu 160[1] cha katiba kinatoa uhuru huo na uwezo wa idara hiyo.

Idara ya mahakama pia lazima ipiganie kubuniwa kwa wakfu wa idara hiyo kama ilivyoashiriwa katika kifungu cha 173, hatua ambayo itahakikisha uhuru wa operesheni za Idara hiyo.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post