Hisia mseto zatolewa kuhusiana na ushindi wa Raisi nchini Iran
Marekani imesema inasikitika kwamba raia nchini Iran hawakuweza kushiriki katika uchaguzi ''huru na haki'' wakati wa uchaguzi wa rais nchini humo.Katika kauli ya ya kwanza kutoka Marekani kuhusiana na ushindi wa mhubiri Ebrahim Raisi mwenye msimamo mkali wa kidini, msemaji wa wizara ya mambo ya nje amesema kuwa raia wa nchi hiyo walinyimwa haki ya kuwachagua viongozi wao katika mchakato huru wa uchaguzi. Wakati huo huo, hisia mseto zinaendelea kutolewa kuhusu ushindi huo wa Raisi huku Israel ikisema kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kuwa na wasiwasi kutokana na ushindi wake kwa sababu ya kujitolea kwake kuendeleza haraka mpango wa kijeshi wa nyuklia. Katika ujumbe kupitia mtandao wa twitter, msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje ya Israel Lior Haiat amesema kuwa kuchaguliwa kwa Raisi kunaweka wazi nia mbaya ya Iran na jamii ya kimataifa inapaswa kuwa na wasiwasi. Raia wengi wa Iran walisusia kura hiyo baada ya wagombea wengi kuenguliwa katika kinyang'anyiro hicho na kusalia na wawaniaji saba pekee.