Iran yasema uchaguzi wa Ijumma ni "mapambano makali"
Katika mkesha wa siku ya uchaguzi wa rais unaotazamiwa kumpa ushindi mgombea mwenye msimamo mkali nchini Iran Ebrahim Raisi, Baraza la usimamizi linalowachuja wagombea limesisitiza kuwa mchuano huo wa kisiasa ni mzito. Abbas Ali Kadkhodaee, Mkuu wa Baraza hilo lenye wajumbe 12 amesema tayari vyombo vya habari na watu wa Iran wamethibitisha kuwa mapambano ni makali na takriban watu milioni 60 wamesajiliwa kupiga kura. Uchaguzi huo unamtafuta mrithi wa rais anaemaliza muda wake Hassan Rouhani ambaye hawezi kugombea tena baada ya kuiongoza nchi kwa mihula miwili ya miaka minne na anaetarajiwa kuondoka madarakani mwezi Agosti. Hata hivyo ushiriki wa wapiga kura unatarajiwa kuwa mdogo katika taifa hilo ambalo wengi wamekatishwa tamaa na miaka mingi ya mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na vikwazo vya uchumi vilivyowekwa na Marekani.

