Israel imesema kuwa imeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo lengwa ya Hamas katika ukanda wa Gaza, kama njia moja ya kujibu kurushwa kwa maputo ya moto kuelekea upande wake .
Milipuko ilisikika katika mji wa Gaza alfajiri ya jumatano .
Maputo kadhaa ya moto yalirushwa kutoka upande wa Gaza kuelekea Israeli mapema Jumanne na kusababisha milipuko kadhaa kulingana na huduma ya zimamoto ya Israeli.
Hii ikiwa ni milipuko ya kwanza tangu kusitishwa kwa vita vilivyoendelea kwa siku 11 kati ya pande hizo mbili Mei 21.
Hilo limefuatia maandamanao yaliyofanywa na raia wa Kiyahudi katika eneo lililokaliwa la Jerusalem Mashariki Jumanne, ambayo yalikuwa yametishia upande wa Hamas, kundi la wanamgambo linaloendesha ukanda wa Gaza.
Tunajua nini kuhusu mashambulizi hayo?
Katika taarifa, wanajeshi wa ulinzi wa Israeli (IDF) walisema kuwa ndege za kivita zilivamia maeneo ya kijeshi yanayoendeshwa na Hamas katika miji ya Khan Yunis na Gaza
Pia taarifa hiyo imeongeza kuwa "shughuli za kigaidi" zilifanyika eneo hilo na kwamba wanajeshi wa Israeli walikuwa wamejitayarisha kwa "matukio yoyote yale, ikiwemo kuanza tena kwa mapigano kati yao ikiwa vitendo vya kigaidi kutoka upande wa Gaza vitaendelezwa".
Haikujulikana mara moja kama mashambulizi hayo ya anga yalisababisha majeruhi wowote.
Msemaji wa kundi la Hamas amesema katika taarifa yake kupitia mtandao wa Twitter kwamba raia wa Palestina wataendeleza "upinzani kwa dhati yote na kutetea haki zao na maeneo matakatifu" huko Jerusalem.
Huduma ya zimamoto ya Israeli ilisema maputo yanayolipuka yaliyorushwa mapema kutoka upande wa Gaza yalikuwa yamesababisha moto kwa maeneo yasiyopungua 20 katika maeneo ya jamii za kusini mwa Israeli.

