Israel ipo katika maandalizi ya kuapishwa kwa serikali mpya ambayo itamfanya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuwa upande wa upinzani baada ya miaka 12 madarakani na uwepo wa mzozo wa kisiasa katika chaguzi nne ndani ya kipindi cha miaka miwili.Naftali Bennet, kiongozi wa chama kidogo cha siasa kali za kizalendo atachukua nafasi ya uwaziri mkuu. Lakini akitaka kuendelea kudumu katika nafasi yake hiyo atapaswa kudumisha umoja wa vyama vya kisiasa na vyama vingine vya mirengo ya kulia, shoto na kati. Netanyahu, ambae anakabiliwa na mashitaka ya rushwa atasalia kuwa kiongozi wa chama kikubwa bungeni na anatarajiwa kuipinga vikali serikali mpya.Serikali mpya ya Israel imeahidi kurejesha hali ya kawaida baada ya sintofahamu ya miaka miwili iliyotokana na chaguzi nne, siku 11 ya vita vya Gaza mwezi uliopita na kadhia ya janga la corona ambalo imeuvuruga uchumi wa taifa hilo kabla haijadhibitiwa kwa kiasi kikubwa na kampeni iliyofanikiwa ya chanjo.
