Mkutano wa kilelele wa siku tatu wa mataifa yenye nguvu kubwa ya uchumi wa kiviwanda duniani, G7 leo hii umefikia siku yake ya mwisho nchini Uingereza kwa kutoa wito wa haraka kusitishwa mzozo wa jimbo la Tigray, huko kaskazini mwa Ethiopia sambamba na ahadi ya chanjo bilioni 1 dhidi ya virusi vya corona kwa mataifa masikini.Pamoja na masuala mengine kadhaa taarifa ya pamoja ya mkutano wa viongozi hao inaonesha wasiwasi mkubwa kufuatia mzozo unaoendelea katika jimbo la Tigray na ripoti zinaeleza kutokea janga kubwa la kiutu. Taarifa hiyo inatoa wito wa kusitishwa uhasama mara moja, kuruhusiwa misaada ya kiutu na kuondoshwa kwa vikosi vya Eritrea.Katika hatua nyingine Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema viongozi hao wa G7 wametoa ahadi ya kuchangia dozi bilioni 1 ya chanjo ya Covid-19 kwa matiafa masikini.Uingereza itatoa kiasi cha chanjo milioni 100, ambacho kitajumuishwa katika mpango mganyanyo wa chanjo unaongwa mkono na Shirika la Afya duniani WHO, ujulikanao kama Covax
