Waziri mkuu wa Israel anasema kwamba jamii ya kimataifa inafaa kuamka kufuatia uchaguzi wa rais mpya wa Iran.
Naftali Bennet amesema kwamba utawala wa Iran umekuwa ukitaka silaha za kinyuklia - kitu ambacho Iran inakana.
Ebrahim Raisi alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Iran siku ya Jumamosi. Alikuwa jaji wa Iran na ana fikra za kihafidhina.
Katika taarifa baada ya ushindi wake , aliahidi kuimarisha imani ya raia kwa serikali ya taifa hilo na kuwa kiongozi wa nchi yote.
"Nitaunda serikali inayofanya kazi kwa bidii, ya mapinduzi na ya kupambana na ufisadi," vyombo vya habari vya serikali vilimnukuu akisema''.
Uchaguzi wote ulionekana kumpendelea bwana Raisi.
Rais huyo mteule ambaye ataapishwa mwezi Agosti yuko chini ya vikwazo vya Marekani na amehusishwa na unyongaji wa wafungwa wa kisiasa wa zamani.
''Katika mkutano wa baraza la mawaziri siku ya Jumapili, bwana Bennett aliambia wenzake kwamba huu ndio wakati wa jamii ya kimataifa kuamka na kuelewa aina ya mtu wanayefanya biashara naye. ".
''Utawala wa mnyongaji haufai kuruhusiwa kumiliki silaha za maangamizi''.
Iran na Israel zimekuwa zikipigana vita baridi , hali iliosababisha mataifa yote mawili kukabiliana lakini yote yakizuia kutokea kwa vita vitakavyoshirikisha mataifa mengine.
Hivi majuzi , hatahivyo , uadui kati ya mataifa hayo mawili umeongezeka tena. Hali ni ngumu , lakini chanzo kikuu cha wasiwasi uliopo ni vitendo vya kinyuklia vya Iran.
Iran inalaumu Israel kwa muaji ya mwanasayansi wake mkuu mwaka uliopita na shambulio katika kinu chake cha madini ya Uranium mwezi Aprili.
Israel haiamini kwamba mpango wa kinyuklia wa Iran ni wa amani na ina ushahidi ina mipango ya kutengeneza silaha za kinyuklia.