Jeshi la Israel limesema litasitisha mpango wake tata wa kufanya uvamizi nyakati za usiku katika makazi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi yanayolenga kukusanya taarifa kuhusu nyumba hizo na wakaazi wake. Jeshi katika siku za nyuma liliutetea utaratibu huo, kama hatua muhimu ya kupambana na makundi ya wanamgambo. Lakini makundi ya haki za binaadamu yanasema sera hiyo inatumika tu kwa kuwatisha raia. Chini ya mpango huo, wanajeshi huvamia majumba ya watu nyakati za usiku ili kuchukua taarifa kuhusu ukubwa wa nyumba na wakaazi wa eneo hilo linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi.
