Home bongo habari Kazi mbili za Rais Samia Mwanza leo
Kazi mbili za Rais Samia Mwanza leo
ben
June 15, 2021
Mwanza . Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anahitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Mwanza leo Jumanne Juni 15, 2021 kwa kushiriki matukio makubwa mawili.
Kabla ya kukutana na vijana wa Mwanza kwa niaba ya vijana wote nchini katika mkutano unaotarajiwa kufanyika uwanja wa michezo wa Nyamagana, kiongozi mkuu huyo wa nchi atashuhudia tukio la utiaji saini wa mikataba mitano ya uendelezaji na maboresho ya usafirishaji kwa njia ya maji.
Miradi hiyo mitano inayohusu ujenzi wa meli mpya ya mizigo na abiria na ukarabati wa meli za zamani unagharimu zaidi ya Sh438.8 bilioni.
Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa Kampuni ya Meli nchini (MSCL), Philemon Bagambilana ametaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa meli mpya ya mizigo ndani ya Bahari ya Hindi na meli mpya ya abiria na mizigo ndani katika Ziwa Tanganyika.
“Mkataba wa tatu utakaoshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni ujenzi wa meli ya mizigo ndani ya Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli ya kusafirisha mabehewa ndani katika Ziwa Victoria na ukarabati wa meli ya mizigo ya Mv Umoja inayotoa huduma ndani ya Ziwa Victoria,” amesema Bagambilana.
Kwa mujibu wa taarifa yake kwa umma iliyotolewa na Bagambilana inaeleza kuwa Samia pia atafanya uzinduzi wa meli mpya ya New Mv Victoria iliyokarabatiwa kwa gharama ya zaidi ya Sh22 bilioni na kuirejeshea upya kwa zaidi ya asilimia 80 baada ya kufungiwa injini mbili mpya na mitambo ya kisasa ya kuiendesha ambayo tayari imeanza kutoa huduma ya kusafirisha abiria na mizigo kati ya Jiji la Mwanza na mji wa Bukoba.
Mkuu huyo wa nchi pia atazindua meli ya Mv Butiama ambayo pia imekarabatiwa kwa zaidi ya Sh5 bilioni, meli hiyo tayari imeanza kutoa huduma.
Akiwa eneo la Bandari ya Mwanza Kusini, kiongozi mkuu huyo wa nchi pia atazindua chelezo iliyojengwa kwa zaidi ya Sh36 bilioni ambayo tayari imeanza kutumika kujenga meli mpya ya Mv Mwanza “Hapa Kazi Tu” yenye uwezo wa kubeba abiria 1, 200, tani 400 ya mizigo na magari 20.
Akizungumza jana Jumatatu Juni 14,2021 wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande cha tano cha reli ya kisasa (SGR) kutoka Mwanza hadi isaka Shinyanga, Rais Samia amesema maboresho ya huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia ya maji, anga na reli katika ukanda wa Ziwa Victoria, hasa Mkoa wa Mwanza unalenga kufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara Afrika Mashariki na Kati.
Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali pia inajenga meli mpya na kukarabati za zamani na kupanua uwanja wa ndege wa Mwanza kuipa mkoa huo sifa ya kuwa kitovu cha biashara kitaifa na kimataifa.
“Hii itatupa sifa ya ushindani wa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati…, tunataka Mwanza iwe kitovu cha biashara kwa nchi za ukanda wa Maziwa Makuu,” amesema Rais Samia.
Awali, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRC), Masanja Kadogosa alimweleza mkuu huyo wa nchi kuwa Mamlaka ya Bandari (TPA) inatekeleza mradi wa ujenzi wa bandari kavu eneo la Fela kwa ajili ya kuhifadhi mizigo itakayosafirishwa kupitia SGR.
“Kwa kujenga bandari kavu Fela ni dhahiri Bandari ya Dar es Salaam itahamia Mwanza na hivyo wafanyabiashara kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani ya Uganda kwa kupokea mizigo yao Mwanza badala ya kusafiri umbali wa zaidi ya kilimeta 1, 300 kuifuata Dar es Salaam,” amesema Kadogosa.