Licha ya kudumu kwa miongo kadhaa, uhasama huo uliibua mapigano maalumu yaliyodumu kwa siku sita na kuweka historia ya aina yake.
Historia ya mzozo wa Israeli na Palestina si ya leo wala jana. Ilianza pale Taifa la ya Israel lilipoanzishwa Ijumaa ya Mei 14, 1948.
Ingawa kulikuwa na matukio mengi yaliyozusha mapambano kati ya Waisrael na Wapalestina kuanzia mwishoni mwa karne ya 19, vita kubwa ya kwanza kati ya Waisrael na Waarabu ni ya mwaka 1947—49. Ingawa vita hiyo iliitwa ‘Vita ya Waarabu-Israeli ya 1948’, ilianza mwaka 1947 na kumalizika rasmi Machi 1949. Ilikolea zaidi lilipotangazwa Taifa la Israel.
Hali hiyo ilichochewa na uhasama uliokuwepo tangu mwaka 1920 ambao uliendelea kwa muda wote hadi ulipogeuka na kuwa vita kamili. Hadi leo uhasama huo haujaisha, na hivyo mzozo nao haujaisha.
Suala la ardhi ndilo lilikuwa chanzo kikuu cha mzozo huo ambao umekuwapo kwa miongo kadhaa sasa.
Uingereza ilichukua na kudhibiti eneo linalojulikana kama Palestina baada ya mtawala wa eneo hilo la mashariki ya kati, Mfalme wa Himaya ya Ottoman, Osman I (pia aliitwa Osman Gaz), kushindwa katika Vita vya Kwanza vya Duniani (WWI- 1914-18). Ufalme huo ulidumu kwa miaka 78, kuanzia mwaka 1844 hadi 1922.
Ardhi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Wayahudi walio wachache na Waarabu walio wengi. Uhasama baina ya makundi hayo mawili ulianza wakati jamii ya kimataifa ilipoipatia Uingereza jukumu la kuwapatia makazi Wayahudi katika eneo la Wapalestina.
Kabla ya hapo kulikuwa na kile kilichoitwa ‘Mpango wa Uingereza kwa Uganda’ ambao dhumuni lake lilikuwa ni kutoa sehemu ya Afrika Mashariki iliyokuwa chini ya Uingereza kwa Wayahudi kama nchi yao. Wazo hilo lilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1903 na Katibu wa Kikoloni wa Uingereza, Joseph Chamberlain kwa kikundi cha Wazayuni cha Theodore Herzl. Hata hivyo mpango huo haukuendelea.
Kwa upande wa Wayahudi eneo la Palestina lilikuwa la mababu zao, lakini Waarabu wa Wapalestina pia nao walidai kumiliki ardhi hiyo na hivyo wakapinga mpango huo.
Kati ya mwaka 1920 hadi wakati wa kumalizika kwa Vita Kuu vya pili vya Dunia (WWII-1939 -1945), idadi ya Wayahudi iliyowasili katika eneo hilo iliongezeka. Wengi wa hawa ni wale waliokimbia mateso barani Ulaya wakitoroka kuuawa wakati wa WWII.
Kutokana na hilo, ghasia kati ya Wayahudi na Waarabu na dhidi ya utawala wa Uingereza ziliongezeka. Ndipo mwaka 1947 Umoja wa Mataifa ulipiga kura kwa Palestina kugawanywa kati ya mataifa ya Wayahudi na Wapalestina huku mji wa Jerusalem ukiwa mji wa kimataifa.
Mpango huo ulikubaliwa na Wayahudi lakini ukakataliwa na Waarabu na haukutekelezwa. Mwaka 1948, baada ya kushindwa kutatua mzozo huo, watawala wa Uingereza waliondoka katika eneo hilo na viongozi wa Kiyahudi wakatangaza kuanzishwa kwa Taifa la Israel.
Wapalestina wengi walipopinga hatua hiyo, vita vikaanza. Wanajeshi kutoka mataifa jirani ya Kiarabu walivamia. Mamia ya maelfu ya raia wa Kipalestina walitoroka na wengine kulazimishwa kutoka katika makazi yao.
Vita hivyo vilianza siku moja baada ya Israel kujitangazia Taifa lake, Jumamosi Mei 15, 1948. Hatimaye vita hiyo ilimalizika Alhamisi Machi 10, mwaka uliofuata, 1949, huku Israel ikiwa imedhibiti eneo kubwa.
Kwa upande wa Jordan, Israel iliteka sehemu ambayo baadaye ilikuja kujulikana kama Ukingo wa Magharibi (West Bank) na kwa upande wa Misri ikilinyakua eneo la Ukanda wa Gaza.
Yerusalemu iligawanywa kati ya wanajeshi wa Israel waliopo magharibi na wanajeshi wa Jordan waliopo mashariki.
Kwa kuwa hakukuwapo na mkataba wa amani, kila upande uliulaumu mwingine, na kwa sababu hiyo vita viliendelea kwa miongo kadhaa.
Vita vya siku sita
Ukiacha mapigano ya mwaka 1948, vita vingine baina ya nchi hizo, vilizuka mwaka 1967. Hivi viliitwa ‘Vita vya siku sita’ ambavyo vilianza Jumatatu Juni 5, 1967 na kumalizika Jumamosi Juni 10, 1967. Vita hii ndiyo simulizi tutakayozungumzia kwenye mfululizo wa makala hizi.
Katika Vita vya siku sita, Israel ililiteka eneo la mashariki mwa Jerusalem na lile la Ukingo wa Magharibi pamoja na eneo kubwa la milima ya Golan iliopo Syria, ukanda wa Gaza na Rasi ya Sinai iliyopo Misri.
Wakimbizi wengi wa Palestina wanaishi katika eneo la Gaza na Ukingo wa Magharibi pamoja na mataifa jirani ya Jordan, Syria na Lebanon.
Wakimbizi hao na wajukuu wao hawakuruhusiwa na Israel kurudi katika makazi yao kwa sababu iwapo wangerudi, nchi hiyo ingeizidi nchi yao na kutishia uwepo wake kama taifa la Wayahudi.
Israel bado imeendelea kulidhibiti na kulikalia eneo la Ukingo wa Magharibi. Ingawa iliondoka katika Ukanda wa Gaza, bado Umoja wa Mataifa unalitambua eneo hilo kama eneo lililotekwa.
Israel inadai kuimiliki Yerusalem kama mji mkuu wa Israel huku Palestina ikidai kuwa eneo la Mashariki ya mji huo ndiyo itakayokuwa mji mkuu wa Taifa la Wapalestina. Hata hivyo, ni Marekani pekee inayotambua kwamba Jerusalem ni eneo la Israel.
Kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, Israel imekuwa ikijenga makazi katika maeneo hayo ambayo kwa sasa yanakaliwa na zaidi ya Wayahudi 600,000. Kwa upande mwingine, Palestina inasema makazi hayo ya Wayahudi ni haramu na ni kinyume cha sheria ya kimataifa na kikwazo cha kuleta amani.
Hali ya wasiwasi na mashaka ni ya kiwango cha juu kati ya raia wa Israel na Wapalestina wanaoishi mashariki mwa Yerusalem, katika eneo la Gaza na lile la Ukingo wa Magharibi.
Gaza inatawaliwa na kundi la wapiganaji wa Kipalestina kwa jina Hamas, ambalo mara nyingi linapambana na wanajeshi wa Israel.
Israel na Misri wanadhibiti eneo la mpakani la Gaza ili kuzuia silaha kusafirishwa hadi kwa wapiganaji wa Hamas.
Raia wa Palestina wanaoishi Gaza na Ukingo wa Magharibi wanadai kuwa wanateswa na vitendo vya Israel, hususan vikwazo.
Kwa upande mwingine, Israel inasema inatekeleza vitendo hivyo kwa lengo la kujilinda dhidi ya ghasia za Palestina.
Raia wa Palestina wamekuwa wakifanya maandamano, wakitaka wakimbizi kurudi katika makazi yao katika eneo ambalo sasa Israel inadai ni lake. Lakini Waisrael wanadai waandamanaji hao wanatumika kama ngao ili kuwashambulia.
Makumi ya raia wa Kipalestina wameuawa na wanajeshi wa Israel ambao wanasema wanachukua hatua hiyo kujilinda.
Hata hivyo, yako mambo kadhaa ambayo Israel na Palestina haziwezi kukubaliana. Hayo ni pamoja na hoja za ni nini hatima ya wakimbizi wa Palestina, au ikiwa makazi ya Wayahudi ya Ukingo wa Magharibi yanafaa kuondolewa ama la, au kama Waisrael na Wapalestina wanaweza kuutumia kwa pamoja mji wa Yerusalem au kama wote wanaweza kuishi kwa amani katika nchi ileile moja.
Mazungumzo ya amani yamekuwa yakifanyika kwa zaidi ya miaka 30, lakini kufikia sasa hakuna suluhu ya mzozo huo. Pamoja na yote hayo, endelea kufuatilia simulizi ya historia hii uone nini kilijiri katika vita vya siku sita kati ya Waisrael na Waarabu.