Kim Jong Un aapa kuwa tayari kwa makabiliano na Marekani

 

Kim Jong Un aapa kuwa tayari kwa makabiliano na Marekani

Rais wa Korea kaskazini Kim Jong Un ameiamuru nchi yake kuwa tayari kwa yote mawili - mazungumzo na makabiliano - na utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani.


Nordkorea Kim Jong Un

Shirika la habari la serikali ya nchi hiyo, KCNA, liliripoti kauli ya kiongozi huyo siku ya Ijumaa (18.06.2021) siku chache baada ya Marekani na mataifa mengine kuihimiza nchi hiyo kuachana na mpango wake wa nyuklia na kurudi kwenye mazungumzo. Baadhi ya wataalamu wanasema kauli ya Kim inaonesha kuwa ana uwezekano wa kushinikiza kuimarisha silaha zake za nyuklia na kuongeza shinikizo kwa Marekani kuachana na kile ambacho Korea Kaskazini inazingatia kuwa sera ya uhasama kwa nchi hiyo,ijapokuwa piaataandaa kuanza tena kwa mazungumzo.

Wakati wa mkutano uliokuwa ukiendelea wa chama tawala siku ya Alhamis, Kim alichambua kwa makini mwelekeo wa sera za Marekani chini ya Rais Biden na kufafanua hatua za kuchukuwa katika uhusiano na Marekani.

Mnamo mwaka 2018, Kim alishiriki mazungumzo mara kadhaa na aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu hatua ya Korea Kaskazini kuendelea na silaha zake za nyuklia. Lakini mazungumzo hayo yalisambaratika baada ya Trump kukataa wito wa Kim wa kuondolewa kwa vikwazo vikali ili aweze kuachana na sehemu ya mpango wake wa nyuklia. Utawala wa Biden umeanzisha mbinu mpya ya kufuatilia mpango wa nyuklia wa Korea Kasakzini ambayo imeitaka kuwa iliyosawazishwa na inayoweza kutumika.

Maelezo kuhusu mbinu hiyo hayajachapishwa lakini maafisa wa Marekani wamependekeza kuwa Biden atatafuta usawa kati ya mikutano ya moja kwa moja kati ya Kim na Trump na uvumilivu wa kimkakati wa aliyekuwa rais, Barack Obama, katika kukabiliana na mpango wa nyuklia wa Kim. Mapema wiki hii, viongozi wa kundi la mataifa saba yenye ushawishi zaidi duniani, G7, walitoa taarifa ya kutaka kusitishwa kabisa kwa mpango wa nyuklia na mipango ya makombora katika Rasi ya Korea. Viongozi hao walitoa wito kwa Korea Kaskazini kurudi tena katika mazungumzo.

Mjumbe wa Marekani kuzuru Korea Kusini

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema mjumbe wake kuhusu Korea Kaskazini, Sung Kim, anatarajiwa kufanya ziara nchini Korea Kusini siku ya Jumamosi kwa mkutano wa mataifa matatu na maafisa wa Korea Kusini na Japan. Ziara hiyo inasisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pande hizo tatu katika kuhakikisha kukatizwa kwa mpango wa nyuklia katika rasi ya Korea.

Hivi karibuni, Kim alitishia kuongeza uwezo wa nchi yake wa nyuklia na kutengeneza silaha za teknolojia ya hali ya juu zinazolenga Marekani bara iwapo taifa hilo litakataa kuondoa vikwazo vyake vikali dhidi ya nchi yake. Wiki iliyopita, Kim alisema kuwa jeshi la Korea kasakzini lazima liwe macho kulinda usalama wa kitaifa.

Nchini China, msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Zhao Lijiang, ametoa wito wa kurejelewa kwa mazungumzo kati ya Korea kaskazini na Marekani na kusema kuwa wanaamini Rasi ya Korea inakabiliwa na awamu mpya ya mvutano.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post