Maafisa 5 wa kutoa chanjo ya polio wauawa Afghanistan
Maafisa wapatao watano wa kutoa chanjo dhdi ya ugonjwa wa kupooza, polio, wamepigwa risasi na kuuliwa mashariki mwa Afghanistan hivi leo. Msemaji wa jeshi la polisi mkoa wa Nangarhar, Farid Khan, amesema wafanyakazi hao wameshambuliwa katika maeneo matatu tofauti katika saa chache kwenye mashambulizi ya kupangwa. Khan aidha amesema hiyo ni kazi ya kundi la Taliban kuwashambulia maafisa wa afya ili kuwanyima watu chanjo dhidi ya ugonjwa wa kupooza. Msemaji wa wizara ya afya ya Afghanistan, Osman Taheri, amethibitisha kutokea mashambulizi hayo. Kundi la Taliban limekanusha kuhusika na hujuma hizo. Afisa wa cheo cha juu wa Umoja wa Mataifa, Ramiz Alakbarov, ameyalaani vikali mashamblizi hayo. Ugonjwa wa kupooza umetokomezwa kote ulimwenguni isipokuwa Afghanistan na Pakistan, ambako watu hawana imani na chanjo na wana wasiwasi kuhusu kampeni za kuutokomeza.
