Ufaransa kuendelea kutumia nishati ya nyuklia
Waziri wa Mazingira wa Ufaransa, Barbara Pompili, amesema nchi yake itaendelea kutumia nishati ya nyuklia kwa miaka mingi ijayo. Waziri Pompili ameitoa kauli hiyo alipozungumza na radio ya Ufaransa, France Inter, hivi leo. Matamshi yake yanakuja wakati kampuni ya nishati ya EDF ikitathmini suala linalofungamanishwa na ongezeko la gesi isiyoonesha mabadiliko yoyote ya kemikali katika kinu chake cha nyuklia cha Taishan nchini China. Pompili amesema nishati ya nyuklia inachangia zaidi ya asilimia 70 ya umeme unaozalishwa nchini Ufaransa. Hata hivyo, amesema nishati ya nyuklia siyo aina salama ya nishati kwa mazingira ikizingatiwa uchafu unaotokana na nyuklia. Kampuni ya EDF ilisema siku ya Jumatatu imefahamishwa juu ya ongezeko la gesi katika mtambo nambari moja wa kinu cha Tiashan.
