Maandamano yatarajiwa eneo la mji mkongwe Jerusalem
Israel inajiandaa kwa maandamano mjini Jerusalem baadaye leo, huku kukiwa na hofu ya kutokea tena machafuko mjini humo. Waisraeli takriban 5,000 wenye misimamo mikali ya kizalendo wanatarajiwa kuandamana wakiwa wamebeba bendera za taifa katika eneo la mji mkongwe. Maandamano hayo yameandaliwa na wafuasi wa waziri mkuu wa zamani, Benjamin Netanyahu, ambaye anaendelea kuishinikiza serikali ya waziri mkuu mpya Naftali Benett. Wapalestina wanayaona maandamano hayo kama uchokozi na makundi ya Fatah na Hamas yameitisha siku ya ghadhabu na kisasi. Maafisa 2,000 wa polisi wametumwa kupiga doria katika eneo hilo. Gazeti la Jerusalem Post limeripoti kuwa jeshi la Israel limetuma vikosi vya ziada Ukingo wa Magharibi ambako kuna uwezekano wa machafuko kuenea hadi eneo hilo.
