Watu 15 wauwawa kwenye shambulizi la bomu Somalia
Makuruta wapatao 15 wameuliwa leo wakati mshambuliaji wa kujitoa muhanga alipoishambulia kambi ya mafunzo ya kijeshi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Afisa wa jeshi Mohamed Adan amethibitisha vifo vya maafisa hao kufuatia hujuma hiyo, akisema idadi huenda ikaongezeka. Adan aidha amesema mshambuliaji alikuwa amejificha miongoni mwa makuruta waliokuwa katika foleni nje ya kambi ya Jenerali Dhegobadan wakati mlipuko huo ulipotokea. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na shambulio hilo linaloelezwa kuwa baya kabisa kufanywa Mogadishu katika kipindi cha miezi 18.
