Mjumbe maalumu wa Marekani kwa Korea Kaskazini anatumai kupata jibu la kuridhisha kutoka kwa taifa hilo, baada ya Marekani kupendekeza wafanye mazungumzo wakati wa safari yake ya mjini Seoul.
Sung Kim, mwakilishi maalumu wa Biden kwa Korea Kaskazini, yuko mjini Seoul kwa mazungumzo na maafisa wa Korea Kusini na Japan kuhusu uhusiano unaosuasua kati ya Korea Kaskazini na Marekani kutokana na mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini uliopelekea Marekani kuiwekea nchi hiyo vikwazo.
Mazungumzo hayo yanayozikutanisha nchi tatu, yanafanyika baada ya Kim Jong Un wa Korea Kaskazini wiki iliyopita kutoa wito wa kuongezwa juhudi za kuboresha uchumi wa taifa lake, liloathiriwa vibaya mwaka jana na janga la virusi vya corona, kufungwa kwa mipaka na sasa likiwa linakabiliwa na uhaba wa chakula.
Baada ya kukutana na Noh Kyu-duk, mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Korea Kusini, mjumbe maalumu wa Marekani Sung Kim amesema washirika wake wamesikiliza vyema matamshi ya kiongozi huyo wa Korea Kaskazini na matumaini yao ni kwamba atakubali kufanya mazungumzo na Marekani hivi karibuni.
Sung Kim aliwaambia waandishi wa habari kwamba Korea Kusini na Marekani wataendelea kuwa na ushirikiano wa karibu ili kuimarisha hali katika Rasi ya Korea na kutafuta njia ya kuanza tena mazungumzo na Korea Kaskazini haraka iwezekanavyo.
Kurudi nyuma kwa maendeleo ya kiuchumi ya Korea Kaskazini kulitokana na kuharibika kwa mazungumzo kati ya Kim Jong Un na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mwaka 2019, baada ya kiongozi huyo wa Korea Kaskazini kutaka nchi yake iondolewe vikwazo vya kiuchumi ili naye apunguzi baadhi ya shughuli zake za kinyuklia.
Katika hotuba zake za hivi karibuni, Kim Jong Un ametishia kuimarisha silaha zake za nyuklia na kudai kuwa hatima ya diplomasia na uhusiano wa nchi hizo mbili inategemea ikiwa Marekani itakubali kuaachana na kile alichokieleza kama sera za uhasama.
Maafisa wa Marekani wamesema kwamba Biden atakuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Kim kama alivyofanya Trump lakini pia atatumia busara ya Barack Obama ya kuwa na ustahmilivu. Lakini baadi ya wachambuzi wanasema Korea Kaskazini italazimika kuchukua hatua za kweli za kupunguza shughuli zake za kinyuklia kabla ya Biden kukubali kuiondoshea vikwazo ilivyowekewa na Marekani.