Mshahara wa Kambole unawalipa Chama, Mugalu

0


YANGA imekata tamaa ya kumpata kwa mkopo straika wa Kaizer Chief, Mzambia Lazarous Kambole ambaye walimpandia ndege mpaka Sauzi.

Anataka mshahara wa mwezi ambao ni sawa na ule wa Clatous Chama na Chris Mugalu wa Simba kwa pamoja.

Injinia, Hersi Said ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya usajili wa Yanga akimwakilisha mdhamini GSM, pamoja na kuzungumza nae kwa saa kadhaa baada ya kupata idhini ya klabu, hata hivyo, masharti yake ni mzigo si tu kwa Yanga bali kwa klabu yoyote ya Afrika Mashariki.

Yanga ilikuwa imepania kupata saini ya Kambole na walishazungumza na klabu yake na kuelewana kupeana kwa mkopo na ilikuwa ni suala la mchezaji husika kukubali tu kiwango cha mshahara na kukwea pipa kwenda Dar es Salaam kuanza kazi Jangwani.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya Yanga, injinia anayetekeleza matakwa ya ripoti ya kocha, ameshindwa kuafikiana na matakwa ya Kambole na ameshawaambia viongozi wenzie; “Imeshindikana, tucheki mwingine.”

Habari zinasema Kambole amekubaliana na posho za Yanga na mambo mengine waliyomwahidi lakini akakomaa anataka mshahara wa Dola 10,000 kila mwezi sawa na Sh23 milioni.

“Amekomaa anataka Dola 10,000 na haipungui, sasa huo ni mzigo kwa Yanga na hata klabu yoyote ile ya Afrika Mashariki, huo mshahara hakuna klabu inayoweza kulipa kwa sasa,” alidokeza kiongozi huyo wa Yanga na kusema wameafikiana kuchana na dili hilo na sasa wameelekeza ndoano zao kwingine.

Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini ndani ya kikosi cha sasa cha Yanga hakuna mchezaji anayelipwa wala kukaribia kiwango anachotaka Kambole ambaye Yanga walipania kumchukua kwa maelezo uwezo wake ni sawa na straika Mkongomani waliyemuuza Horoya ya Guinea, Heritier Makambo.

Mshahara anaotaka Kambole ndani ya Yanga pale Simba unalipa mastaa wakubwa wawili ambao ni tegemeo kwenye kikosi cha kwanza, Chama na Mugalu kwa mwezi mmoja.

Jambo ambalo limewafanya Yanga kufikiria mara mbili na kuamua kuachana nae hasa wakiangalia ubora wa Chama na Mugalu wamekuwa na msaada mkubwa kwenye kikosi cha kwanza tofauti na Kambole ambaye kwenye miezi ya hivi karibuni alikosa namba kikosini kutokana na kile kilichodaiwa kocha hamkubali.

Hata hivyo pamoja na sababu hiyo, Mwanaspoti limedokezwa Kocha mpya wa Kaizer, Stuart Baxter amemwambia Kambole pia asiondoke kwani ataanza kumpa nafasi ya kucheza kwa vile yeye ndiye aliyemsajili awali kabla hajapigwa chini na kurudishwa sasa.

Baxter ndiye kocha mpya wa Kaizer akichukua nafasi ya Gavin Hunt aliyetimuliwa siku chache baada ya kuwang’oa Simba hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

About Us

Light Speed Template is Designed Theme for Giving Enhanced look Various Features are available Which is designed in User friendly to handle by Piki Developers. Simple and elegant themes for making it more comfortable