Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi amewaambia viongozi anataka wachezaji nane wapya.
Yanga tayari imeshamalizana na beki Djuma Shaban wa AS Vita akija kama beki wa kulia kupambana na Kibwana Shomari aliyecheza mechi nyingi msimu huu.
Mbali na Djuma pia Mwanaspoti linajua Yanga inamalizana na beki wa kushoto wa KMC, Brayson Raphael lakini pia wakitafuta kwa siri beki wa maana wa kati ambaye kama atapatikana kuna uwezekano wakaachana na nahodha wao Lamine Moro ambaye kwenye siku za karibuni amechafuka kinidhamu.
Mwanaspoti linafahamu Yanga inakaribia kumalizana na kiungo Mercey Vumbi Ngimbi, nahodha wa Union Maniema iliyomaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu nchini DR Congo akiwa pia katika timu ya taifa.
Hesabu za usajili wa winga mzawa, akili ya mabosi wa Yanga zipo kwa Dickson Ambundo wa Dodoma Jiji ambaye mazungumzo yao bado hayajakamilika lakini yapo kwenye hatua nzuri.
