Serikali yatoa kauli uchaguzi mkuu TFF

0


SERIKALI imevunja ukimya wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utakaofanyika Agosti 7, mkoani Tanga.

Baadhi ya wadau walilalamikia baadhi ya kanuni ikiwamo kipengele cha kupata wadhamini angalau kuanzia watano wakidai hakina usawa kwa wagombea.

Naibu Katibu Mkuu, wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Ally Possi amesema mchakato huo utaendelea kwa kanuni na taratibu za TFF.

“Kamati ya uchaguzi imefafanua kila kitu, hivyo uchaguzi wa TFF utafanyika kwa kanuni na taratibu za shirikisho hilo,” alisema.


BMT YANENA

Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Neema Msita ameeleza kupokea baruapepe kutoka kwa mdau wa soka akilalamikia baadhi ya vipengele kwenye Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

“BMT ni chombo kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria na kipo kwa ajili ya kusimamia vyama, klabu pamoja na shirikisho zote za michezo nchini na tumekuwa tukihakikisha kwa kuona vyama na klabu zikijiendesha kwa kuzingatia katiba.

“Tunaelewa sasa hivi vyama vingi pamoja na klabu zinaendelea na uchaguzi ikiwemo TFF, hivyo wito wetu kwa shirikisho na wadau wote kuhakikisha wanafanya mambo yao kwa kufuata katiba,” alisema Neema.

Aliongeza kama kutatokea makosa yoyote vyombo vya serikali vipo macho na wasisite kutoa taarifa ili kuona haki inatendeka.

Alisema wao wanaisajili katiba baada ya kupata maoni ya wadau, hivyo yanapojitokeza maoni ya namna hii wana mamlaka ya kutengua baadhi ya vitu wakati wa usajili wa katiba. Uchaguzi mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika Agosti 7, mwaka huu huko Tanga.


MGONGOLWA, ZITTO WATOFAUTIANA

Mwanasiasa, Zitto Kabwe na mwanasheria Alex Mgongolwa wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya uchaguzi huo hasa kwenye kipengele cha udhamini kwa wagombea kilichoibua sintofahamu.

Wakati Zitto akisisitiza ni kanuni inayomtengenezea mazingira mgombea fulani sanjari na kutengeneza uadui, Mgongolwa amesema ni kipengele kinachoonyesha ni kiasi gani unaungwa mkono.

“Kila kanuni kwenye sheria ina mantiki, kuwa na wadhamini ni dhamira ya kupata uhalali na kuonyesha ni kiasi gani unaungwa mkono, binafsi naona ni sahihi,” alisema Mgongolwa.

Zitto kwa upande wake alisema “Mkoa fulani ukionyesha kutomuunga mkono rais anayetetea kiti chake, halafu akashinda kwenye uchaguzi, miaka minne akiwa madarakani lazima utanyooshwa ukizingatia mkoa unautegemea uongozi wa kitaifa,” alisema.

Kuhusu elimu kwa wagombea, Mgongolwa aliunga mkono akisisitiza umuhimu wa elimu katika kuongoza shirikisho hilo akishauri wadau kutofanya jitihada kupingana na kipengele hicho.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

About Us

Light Speed Template is Designed Theme for Giving Enhanced look Various Features are available Which is designed in User friendly to handle by Piki Developers. Simple and elegant themes for making it more comfortable