Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inadai kwamba wanajeshi kutoka Somalia walipigana kwa ushirikiano na Waeritrea katika eneo linalokumbwa na mzozo la Ethiopia-Tigray.
Ripoti ya Mwakilishi Maalum wa Umoja wa mataifa Mohamed Abdelsalan Babiker ilisema wanajeshi wa Somalia walipigana katika mstari wa mbele huko Tigray.
"Mbali na ripoti za kuhusika kwa wanajeshi wa Eritrea katika mzozo wa Tigray, mwakilishi huyo Maalum pia alipokea habari na ripoti kwamba wanajeshi wa Somalia walihamishwa kutoka kambi za mafunzo ya kijeshi huko Eritrea hadi mstari wa mbele huko Tigray, ambapo waliandamana na wanajeshi wa Eritrea wakati wakivuka mpaka wa Ethiopia, "inabainisha ripoti hiyo.
Ilisema kwamba wapiganaji wa Somalia waliripotiwa kuwapo katika mji mtakatifu wa Ethiopia wa Aksum. Serikali ya Somalia imekanusha kuhusika katika mzozo wa Tigray.
Eritrea haikushirikiana katika uchunguzi wa UN ambao ulizingatia zaidi hali ya haki za binadamu huko Eritrea.
Mwakilishi wa wa UN alisema ripoti yake ilitokana na uchunguzi na habari kutoka vyanzo tofauti.
Mnamo Februari, Shirika la Amnesty International lilishtumu wanajeshi wa Eritrea huko Aksum kwa kuua mamia ya watu haswa zaidi ya siku mbili mnamo Novemba ambayo inaweza kuwa ni uhalifu dhidi ya binadamu – madai ambayo mamlaka ya Eritrea ilitupilia mbali.
Mzozo wa Tigray uliibuka mnamo Novemba mwaka jana wakati serikali ya Ethiopia ilipoanzisha shambulio la kukiondoa chama tawala cha jimbo hilo TPLF madarakani baada ya wapiganaji wake kuteka kambi za jeshi za serikali huko Tigray.
Tangu mzozo ulipoibuka mwaka jana, maelfu ya watu wanafikiriwa kuuawa na mamilioni wanahitaji msaada wa kibinadamu.
wakati huo huo Serikali ya Ethiopia imeshutumiwa kwa kutekeleza mauaji ya kiholela ya kijana mmoja - katika ripoti mpya ya Human Rights Watch. Amanuel Wondimu Kebede mwenye umri wa miaka 17 aliuawa katika mkoa wa Oromia wa Ethiopia mnamo Mei mwaka jana- ni mmoja wa raia wengi waliokufa tangu mapigano yalipoanza katika eneo hilo miaka 3 iliyopita. Imesababisha wito wa uwajibikaji zaidi kwa vikosi vya usalama nchini humo.
Video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha dakika za mwisho za Amanuel Wondimu Kebede .. Mikono yake ilikuwa imefungwa nyuma yake. Bunduki ilikuwa imetundikwa shingoni mwake ... uso wake ulikuwa na damu wakati alikuwa akizungumza na kamera.
Human Rights Watch inadai kwamba - dakika chache tu baadaye - vikosi vya usalama vya Ethiopia viliamuru kijana huyo ageuze kichwa chake… kabla ya kumpiga risasi mara mbili mbele ya mashahidi wasiopungua wanne.
Wakati huo, ilidaiwa kuwa Amanuel alikuwa amempiga risasi na kumjeruhi mtu mwingine - na vile vile alikuwa akihusishwa na mauaji ya mwandishi wa habari wa huko.
Hili pia limepingwa - na mashahidi wakisema alikuwa mwanafunzi mzuri ambaye alifanya kazi katika kanisa la eneo hilo.
Mzozo wa miaka mitatu kati ya serikali na Jeshi la Ukombozi la Oromo umewaacha raia wengi wamekufa. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanadai udhalilishaji unaofanywa na vikosi vya usalama, pamoja na kuzima kwa mawasiliano na mauaji ya kiholela.
