Vifo vya watu maarufu duniani vimekuwa vikigusa mioyo ya watu wengi, miongoni mwao ni viongozi wa kidini hususan wale wanaotumia televisheni au mtandao kufikisha huduma zao kwa hadhira.
Katika makala haya tunawaangazia baadhi ya Wainjilisti wa televisheni na mtandao ambao vifo vyao viliigusa mioyo ya wengi.
1.Nabii TB Joshua
Kifo cha Mchungaji maarufu wa Nigeria Temitope Balogun Joshua, maarufu TB Joshua kilichotokea tarehe 5 Juni, 2021 ni cha hivi karibuni kilichowagusa wengi duniani
Bw Joshua ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 57, alikuwa maarufu kwa sababu tofauti. Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na ''miujiza'' aliyodaiwa kuifanya kama vile uponyaji, utajiri wake pamoja na ufuasi wa mamilioni ya watu barani Afrika na maeneo mengine ya duniani.
Alikuwa na haiba ya kipekee na wengi waliamini kuwa ''alitumwa'' na Mungu kwa ajili ya kutatua matatizo yao kupitia miujiza.
Hatahivyo baadhi hawakuamini kuwa kweli alikuwa akifanya miujiza na baadhi walimuita ''mwanamazingaombwe'' na ''anayetumia uchawi'' badala ya miujiza ya Mungu.
Kufuatia kifo chake maelfu ya wafuasi wake wamekita kambi kwenye makao makuu ya kanisa lake la Synagogue Church Of All Nations (SCOAN) kuomboleza kifo chake.
2.Mhubiri wa injili Billy Graham
Kifo cha Mhubiri wa injili Billy Graham wa Marekani kilichotokea tarehe 21 Februari, 2018 kilikuwa ni pigo kubwa kwa wengi duniani.
Billy Graham, aliyepata umaarufu mkubwa duniani katika karne ya 20 alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 99.
Graham, alianza kuhubiri jijini London Uingereza mnamo mwaka 1954, na alifahamika kwa sifa ya kukusanya maelfu ya watu kila mahali alipofanya mikutano ya hadhara ya injili tangu miaka ya 50 mpaka kifo chake.
Afrika Mashariki, Graham aliwahi kuhubiri Tanzania, miaka 55 iliyopita, wakati nchi hiyo ikiitwa Tanganyika, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Afrika miaka ya 1960.
Takriban "watu 40,000 walihudhuria mkutano huo wa siku moja, tarehe Feb 28. 1960", kwa mujibu wa mtandao wa shirika lake.
Mwaka 1949, alipata umaarufu wakati alihubiri kwa wiki nane kwenye hema kubwa huko Los Angeles.
Wakati wa harakati za mashirika ya kupigania haki za binadamu, Graham aliibuka kuwa mkasoaji mkubwa wa ubaguzi wa rangi nchini Marekani.
Kwa zaidi ya miaka 60 inakadiriwa kuwa alihubiri kwa jumla ya watu milioni 210.
Mahubiri yake yalipendwa na wengi kutokana na haiba na mvuto kwa wafuasi wake.
Zaidi ya mahubiri pia alifahamika kama Muinjilist ambaye aliheshimiwa si tu kwa wafuasi wake pekee, bali pia hata kwa watu wengine kutokana na haiba yake.
3.Reinhard Bonnke
Bonke Aliwataka waumini wake kuchukua uongozi wa kanisa hilo kutoka kwake
Sawa na Billy Graham, Kifo cha Muinjilisti wa televisheni Reinhard Bonnke, Mchungaji na Muinjilisti aliyekuwa maarufu duniani nyoyo za mamilioni ya watu kote duniani,
Bonnke MMarekani mwenye asili ya Ujerumani ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 79 alifahamika kwa kuvutia umati wa watu kila mahali alipokwenda.
Katika taarifa iliiyotolewa na mke wake, Annie Bonnke kwenye ukurasa wake wa Facebook, alisema : Kifo cha mjumbe huyu wa Mungu kimetangazwa na Bw Bonnke amerejea kwa amani kwa Muumbaji wake mbinguni
Kwa miaka 60 iliyopita, Bonnke alikuwa Muinjilisti kote duniani, hususan Afrika, ambako aliandaa mipango ya kuwafikia watu na alikubalika sana na wafuasi wake hasa nchini Nigeria.
Miongoni mwa nchi za Afrika ambazo Bonnke alizitembelea ni pamoja na Nigeria, Kenya, na Zimbabwe.
4.Mchungaji Getrude Rwakatare
Mchungaji Getrude Rwakatare
Mchungaji Getrude Rwakatare kutoka Tanzania , ambaye alikuwa mchungaji mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto jijini Dar es Salaam na Mbunge wa Viti Maalumu nchini Tanzania aliaga dunia Aprili 20 jijini Dar es Salaam Tanzania.
Bi Rwakatare alikuwa maarufu kupendwa na wafuasi wake kutokana na mtindo wa mvuto wa Mahubiri yake ambapo alichanganya na ucheshi na kutoa mifano halisi ya maisha.
Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa moto alipata umaarufu zaidi kwa maombi yake ya kuwaombea watu wenza wao katika kile alichokiita ''upepo wa kifulifuli'', kauli iliyoenea hata katika mataifa jirani kupitia video za mitandao ya kijamii zilizoonesha wanawake wakikimbilia madhabahu kuombewa ili wapate waume wa kuwaoa.
Kwa mujibu wa familia yake, kifo chake kilisababishwa na shinikizo la damu na matatizo ya moyo. Siku moja baadaye, Spika wa Bunge Job Ndugai akatangaza kuwa mazishi yake yatasimamiwa na serikali na kuwa yatahudhuriwa na watu wasiozidi 10.
5.Mchungaji Mitimingi
Mchungaji Maarufu wa Kanisa la Ghala la Chakula cha Uzima Peter Mitimingi
Usiku wa Mei 3,2020 hautasahaulika miongoni mwa wafuasi na wapenzi wa Mchungaji Maarufu wa Kanisa la Ghala la Chakula cha Uzima Peter Mitimingi aliyefariki dunia baada ya kuugua ghafla.
Mitimingi Kutoka Tanzania alikuwa maarufu kwa mahubiri yake ya mitandaoni nchini humo ambayo yalikuwa yakilenga nyanja mbalimbali za kimaisha kuanzia mahusiano, masomo mpaka ujasiriamali.
Alikuwa na mvuto na haiba ya aina yake katika mahubiri yake. Alichanganya mahubiri na mifano iliyojaa mafunzo na ucheshi, jambo lililomfanya apendwe na kufuatiliwa na hata wale ambao hawakuwa wafuasi wa kanisa lake lake ambao walielezea kuvutiwa na mafunzo yake kupitia mitandao ya kijamii kama vile YouTube.
Pia alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma ya the Voice of Hope Ministry, Mshauri wa Saikolojia wa BLCCC.
6.Mchungaji Myles Munroe
Mchungaji raia wa Bahamas Myles Munroe alifariki dunia katika ajali ya ndege mwaka 2004 alipokuwa akienda kwenye Mkutano wa dunia wa viongozi uliokuwa umeandaliwa na Shirika lake la Myles Munroe International.
Alikuwa mmojawapo wa wachungaji waliokuwa na ufuasi mkubwa na kupendwa na watu mbali mbali duniani kutokana na Mahubiri yake hususan kwa jinsi alivyohusisha Biblia na maisha ya kawaida ya kila siku ya binadamu.
"Bila shaka alikuwa mmoja wa watu maarufu waliotambuliwa kidini kuwahi kuwa nao nchini mwetu," . "Umaarufu wake kama balozi wa Huduma ya Kikristo uliambatana naye kokote alikosafiri duniani , iwe ni katika Caribbean, Marekani, Asia, Ulaya au Afrika'', alisema Waziri Mkuu wa Bahamas alipotangaza kifo chake.
Mchungaji Myles Munroe, aliheshimika na kupendwa si tu na Wakristo bali pia viongozi wa kawaida nchini mwake na kote duniani kutokana na mafunzo yake ya uongozi kwa misingi ya kikristo na utu.
Licha ya kwamba baadhi ya wachungaji hawa hawapo tena duniani, mahubiri yao yanaendelea kuishi na kusikilizwa na wengi kupitia mitandao ya kijamii hususan YouTube.





