Taliban yaitaka Uturuki kuondoa wanajeshi wake Afghanistan
Kundi la wapiganaji la Taliban limekataa pendekezo la Uturuki la kuulinda uwanja wa ndege wa Kabul pindi wanajeshi wa Marekani watakapoondoka nchini Afghanistan. Msemaji wa Taliban Suhail Shaheen amesema Uturuki imekuwa sehemu ya vikosi vya Jumuiya ya kujihami NATO kwa miaka 20, hivyo nayo itapaswa kuondoa vikosi vyake chini ya makubaliano ya mwaka 2020. Hatua hiyo inazusha wasiwasi kwa nchi na mashirika kadhaa ya kimataifa yenye wafanyakazi wake mjini Kabul, kuhusu namna watakavyo waondoa watumishi wake kwa usalama kutoka taifa hilo lililokumbwa na vita. Uturuki ilitoa pendekezo la kuulinda uwanja wa ndege wa Kabul, katika mkutano wa NATO wa mwezi Mei wakati Marekani na washirika wake walipokubaliana kuondoa wanajeshi wake kufikia Septemba 11, baada ya miaka 20 ya kuunga mkono serikali ya Afghanistan katika mapambano na Taliban.

