Serikali ya Ujerumani imetangaza kuwa ipo katika maandalizi ya kupanua wigo wa mchango wake katika kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabia nchi.Katika ukurasa wake wa Twitter, kandoni mwa mkutano wa nchi zilizostawi kiviwanda na tajiri zaidi ulimwenguni za G7 mjini Cornwall Uingereza, msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Seibert ameandika kuwa Ujerumani itatumia Euro bilioni 6 kila mwaka kwa ajili ya ulinzi wa mazingira hadi ifikapo 2025. Kikiwa ni ongozeko la kiwango cha sasa cha Euro biloni 4.Aidha ameongeza kwamba kundi la G7 linapaswa kuwa kinara katika ufadhili wa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi. Lakini msemaji mwingine wa serikali ya Ujerumani amesisitiza kwamba mafanikio ya mkutano wa kilele wa mazingira wa Umoja wa Mataifa wa Glasgow, Scotland, wa Novemba unategemea ahadi zitakazotolewa na mataifa ya G7.

