Ujerumani yawarejesha nyumbani wanajeshi wake kutoka Lithuania
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer amesema Ujerumani itaondoa platuni nzima ya wanajeshi wake walioko Lithuania baada ya wanachama wake kutuhumiwa kwa tabia za kibaguzi na chuki dhidi ya Wayahudi. Madai hayo yanayofungamanishwa na kisa kimoja kilichotokea katika mgahawa mmoja mwezi Aprili yaliripotiwa kwa mara ya kwanza na tovuto ya jarida la Spiegel siku ya Jumatatu. Wanajeshi hao wanadaiwa kuimba nyimbo za ubaguzi na chuki dhidi ya Wayahudi, na mmoja wao pia alidaiwa kumnyanyasa kingono mwenzake alipokuwa amelala, tukio lililoonekana katika mkanda wa vidio. Waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani amesema wanajeshi wote 30 waliopelekwa Lithuania watarejeshwa nyumbani mara moja. Aliandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba tabia ya wanajeshi hao ni fedheha kwa wale wote wanaohudumu katika usalama wa taifa hilo kila siku. Uchunguzi dhidi ya madai hayo tayari umeanzishwa na Kramp-Karrenbauer amesema mwanajeshi atakayepatikana na hatia atawajibishwa.


