Gazeti la Apple Daily lavamiwa na polisi Hong Kong
Polisi mjini Hong Kong imemkamata mhariri Mkuu na watendaji wanne wa gazeti linalotetea demokrasia la Apple Daily, baada ya kuvamia chumba chake cha habari kwa mara ya pili, katika pigo la karibuni zaidi kwa gazeti hilo. Gazeti la Apple Daily na mmiliki wake Jimmy Lai wamekuwa mwiba kwa serikali ya China bara kutokana na uungaji wao mkono usiotetereka kwa vuguvugu la kudai demkorasia na ukosoaji mkali wa viongozi wa kiimla wa China. Zaidi ya maafisa 500 walihusika katika uvamizi huo uliofanyika mapema leo asubuhi ambao serikali inasema ulichochewa na taarifa zilizoandikwa katika gazeti hilo zinazotoa wito wa Hong Kong na viongozi wake kuwekewa vikwazo. Ni mara ya kwanza uvamizi kama huu kufanyika chini ya sheria mpya ya usalama mjini Hong Kong.

