Umoja wa Mataifa wahofia kuongezeka machafuko Afghanistan
Umoja wa Mataifa umesema unajiandaa na uwezekano wa kuongezeka machafuko nchini Afghanistan wakati vikosi vya Marekani vitakapoondoka nchini humo baada ya miongo miwili. Mkuu wa shirika linalohudumia wakimbizi la Umoja huo, UNHCR Philipo Grandi, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba anatambua operesheni za kimataifa za kijeshi haziwezi kudumu wakati wote lakini ameonya kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani na wengine nchini Afghanistan ni ishara kwamba huenda machafuko yakaongezeka tena na wao wanajiandaa na hilo. Wasiwasi kama huo pia ulionyeshwa na rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron hivi karibuni. Wanamgambo wa Taliban wamezidi kujiimarisha kwenye maeneo mengi nchini Afghanistan wakati kikosi cha mwisho cha wanajeshi wa Marekani kikitaraji kuondoka ifikapo mwezi Septemba.
