Zaidi ya wanajeshi 20 wauwawa Kaskazini mwa Afghanistan
Maafisa wa mkoa wa kasikazini wa Faryab wamesema kundi la Taliban limewauwa zaidi ya makomando 20 wa jeshi la Afghanistan. Kulingana na madiwani wa mkoa huo, wanajeshi kutoka kikosi maalumu walipelekewa katika mkoa huo kuikomboa wilaya iliyotekwa na Wataliban takriban siku 10 zilizopita. Madiwani hao, Abdul Manan Qati na Fazal Haq Mohammadi, wamesema vikosi vya usalama vilichukua udhibiti wa wilaya ya Dawlat Abad kutoka kwa Taliban Jumanne jioni, lakini wapiganaji waliokuwa wamejificha katika vijiji vya jirani wakafanya shambulio la kuvizia. Vifaru vya kijeshi visivyopungua viwili viliharibiwa katika milipuko ya mabomu ya kandoni mwa barabara wakati wa shambulio hilo. Vurugu zinaendelea bilo ukomo nchini Afghanistan, na wanamgambo wameshuhudia mkururo wa mafanikio katika siku za karibuni. Tangu kuanza rasmi kwa mchakato wa kuondoa wanajeshi wa Marekani na Nato Mei Mosi, wilaya zisizopungua 27 zimeangukia mikononi mwa kundi la Taliban.

