Mchungaji Ambilikile Mwasapile maarufu kwa jina la 'Babu wa Loliondo', ambaye alipata umaarufu wa kutoa tiba ya dawa ya asili iliyopeanwa kwa kikombe na kudaiwa kutibu magonjwa mbalimbali amefariki dunia.
Gazeti la Mwananchi nchini humo limemnukuu mmoja wa waliokuwa wasaidizi wa mzee huyo, Paul Dudui akisema mzee Mwasapile amefariki ijumaa mchana katika kituo Cha Afya cha Digodigo baada ya kuugua ghafla.
"Ni kweli mzee amefariki muda huu ndio tunasubiri mwili uletwe hapa chumba cha kuhifadhi maiti hospitali ya Wasso" Gazeti hilo limemnukuu Dudui
Kulingana na gazeti hilo Dudui amesema mwili wa mchungaji huyo ulifaa kupokelewa na viongozi wa Serikali wa Wilaya ambao ndio wangetoa taarifa rasmi
"Huu msiba mkubwa kwa wilaya nzima ya Ngorongoro na Kata ya Samunge alipokuwa anaishi mzee kwani ameleta mafanikio makubwa kutokana na kikombe cha dawa alichokuwa anatoa "amenukuliwa na gazeti hilo
Amesema kabla ya kifo chake mzee huyo aliugua wiki iliyopita na kupewa matibabu kisha kurejea nyumbani na leo ndio hali ilibadilika ghafla na kukimbizwa kituo cha Afya cha Digodigo na kufariki.
Mchungaji Mwasapile, mwenye umri wa miaka 86, aligonga vichwa vya habari baada ya maelfu watu kufurika nyumbani kwake kupata tiba asili mwaka wa 2011 . Wakati huo hakuwa akiwataka watu wafurike nyumbani kwake kwa sababu ya idadi kubwa ya watu waliokuwa wamepanga foleni kwa wiki kadhaa kungoja tiba yake .
Vyombo vya habari nchini humo viliripoti wakati huo kwamba takriban watu 52 walifariki dunia wakisubiri kupata tiba yake.
Mwandishi mmoja wa BBC alisema foleni ya watu ilikuwa hadi urefu wa kilomita 26 alipokua katika eneo hilo
Dawa ya Bw Mwasapile ilitengezwa na mitishamba na maji, na wakati huo aliiuza kwa shilingi 500 za Kitanzania.
Alipomtembelea Bw Mwasapile nyumbani kwake eneo la Loliondo mwaka huo wa 2011 mwandishi wa BBC Caroline Karobia aliwakuta watu 6,000 wakimsubiri askofu huyo mstaafu wa kanisa la Kilutherani la Tanzania (ELCT).
Watu walikuwa wakimsubiri kwa siku kadhaa barabarani na nje ya nyumba yake katika kijiji cha Samunge, bila ya kuwa na mahala pa kulala, maji safi wala vyoo ili tu waweze kuipata dawa yake
Wakati tiba yake hiyo ilipoonea , kuna watu waliochukua hatua za kuwatoa ndugu zao hospitalini ili kwenda kwake kupata tiba wakiamini wataponeshwa.
Baadhi ya watu waliripotiwa kufa hata kabla ya kuonana naye.Hizi hapa picha za jinsi hali ilivyokuwa wakati watu walivyofurika kupata dawa y Mzee wa Loliondo
Watu wengi walisafiri kutoka mbali na hata nchi jirani kwenda kupata dawa ya mzee Mwasapile
Kikombe kimoja cha dawa yake kiligharimu shilingi 500 za Tanzania