Mwenyekiti wa chama cha CHADEMA Freeman Mbowe amesema kuwa chama hicho kitaendelea kufanya makongamano ya kudai katiba nchi nzima bila ya kusitisha kwani wanafuata sheria za nchi.
Msimamo huo unakuja siku mbili baada ya jeshi la polisi Mkoani Mwanza kuwakamata baadhi ya wafuasi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo( Chadema) kabla ya kuwaachia hiyo Jumapili na kulizuia kongamano la kudai Katiba mpya lililokuwa limeandaliwa na Baraza la vijana la chama hicho.
Katika siku za hivi karibuni kumeibuka mjadala nchini Tanzania juu ya haja ya kuendelea na mchakato wa kuandika Katiba mpya huku makundi mawili yakiibuka lile linaloona haja ya kuandikwa Katiba mpya na lile linaloona hakuna haja hiyo.
Kupitia mwenyekiti wao, CHADEMA imetangaza siku rasmi ya kufanya kongamano la kudai katiba mpya jijini Mwanza siku ya Jumatano wiki hii, huku wakieleza kuwa vuguvugu la kudai katiba halitasitishwa huku wakisubiri kikao cha kamati kuu ya chama tarehe 31 mwezi huu ambacho kitafanya maamuzi yao kuhusu mikutano ya hadhara.
Mbali na dai la Kuandikwa kwa katiba mpya nchini Tanzania, MBOWE amezungumzia pia juu ya mjadala unaoendelea nchini Tanzania kuhusu tozo za miamala ya simu.
Katika siku za hivi Karibuni, chama cha CHADEMA kimekuwa kikiendesha kampeni za ndani na nje kwa kutumia mitandao ya kijamii kikidai KATIBA MPYA wakati ambao Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwaomba watanzania kumpa muda kwanza kabla ya kuamua mustakabali wa KATIBA ya Tanzania.
Mchakato huo ulifikia hatua ya kupigiwa kura baada ya Bunge la Katiba lililokuwa chini ya Marehemu Samweli Sitta kukamilisha mchakato wake ambao ulipingwa na kususiwa na vyama vya upinzania pamoja na baadhi ya wanaharakati waliokuwemo ndani ya Bunge hilo.