Familia moja nchini Marekani ilipigwa na butwa baada ya kugundua kuwa dola bilioni 50 za Kimarekani zimewekwa kimakosa katika akaunti yao ya benki, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Marekani.
Darren James, 47, anasema alitoka kazini Baton Rouge Jun 12, baada ya mke wake kumuonesha kiwango kikubwa cha fedha katika simu yake.
"Nilishangaa, 'Pesa hizi zimetoka wapi ?'" James alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha FOX Television. "Tulikuwa tukisubiri kubishiwa hodi ... kwasababu hatumjui mtu yeyote aliye na pes kama hizo."
Familia hiyo moja kwa moja iliwasiliana na benki ya Chase, kulingana na baba huyo wa watoto wawili.
James, ambaye aliwahi kufanya kazi katika kitengo cha usalama wa umma huko Louisiana, amesema wazo la kuficha hela hizo na kuzitumia na mtu mwingine halikumjia.
"Tulijua sio pesa zetu. Hatukuifanyia kazi, kwa hivyo hatungefanya lolote," James alisema.
Siku nne baadaye, benki ilirekebisha hitilafu hiyo.
Msemaji wa kampuni hiyo aliiambia televisheni ya FOX katika taarifa iliyotolewa jana kwamba ilikuwa hitilafu ya kimitambo ambayo ilitokea wiki iliyopita na kuathiri akaunti za benko hiyo . "Suala hilo limeshughulikiwa na akaunti hizo zinaonesha fedha sahihi zilizokuwepo."
Lakini James anasema benki hiyo haijamfahamisha jinsi hitilafu hiyo ilivyotokea. Baba huyo pia anahoji ikiwa akaunti yake imedukuliwa.
"Nataka kujua ni nini kilifanyika," aliongeza kusema. Hali kama hiyo inakufanya uwe na hofu kuhusu usalama wa fedha zako. "
Baada ya kisa hicho, James, ambaye sasa amerejea kazini, alisimulia jinsi alivyojihisi kuwa bilionea kwa muda mfupi.
"Nilijisikia vizuri sana," alisema.
James anatarajia hatua yake itawashawishi watu wengine katika jamii kuwa waungwana.