Mama ambaye alimrusha mtoto wake kwa kundi la watu akiwa katika jengo ambalo lilikuwa na moshi wa moto mjini Durban Afrika Kusini ameiambia BBC namna ambavyo anashukuru wale walioweza kumuokoa binti yake.
“Jambo ambalo nililofanya ni kuwaamini watu ambao siwajui kabisa,” Naledi Manyoni alisema, aliongeza kusema kuwa yeye na binti yake Melokuhle wanaendelea vizuri baada ya tukio lile.
BBC ilimpiga picha mama huyo akirusha mwanae mdogo Melokuhle wakati ghasia na uporaji ukiendelea katika mji wa Durban, siku ya Jumanne.
Watu waliokuwa katika maduka ya chini waliwasha moto katika jengo ambalo bi Manyoni alikuwa amemtembelea mshirika mwenzie.
Walikuwa katika gorofa la 16, wakati walipoanza kuhisi kuna moshi .
Lifti zilikuw ahazifanyi kazi kwa sababu ya moto, hivyo bi Manyoni aliamua kutumia ngazi kushuka akiwa na mwanae.
Hata hivyo hakuweza kufika gorofa la chini kwa kuwa kulikuwa na eneo ambalo lilikuwa limezuiwa.
Aliweza kufika kwenye korido la gorofa la pili na kuomba watu wamsaidie kumdaka mwanae.
“Kile nilichokuwa nawaza ni mwanangu aishi ,” alisema.
Zima moto walifika katika eneo la tukio dakika 20 baada ya watu kuanza kuokoa wakazi wa eneo hilo - na hivyo ndivyo bi Manyoni alivyoweza kuwa na mtoto wake.
Aliiambia BBC kuwa alifanikiwa kurudi katika gorofa alilokuwa anaishi saa sita usiku.

